Kimataifa

China yakosoa vita vya Amerika dhidi ya kampuni ya Huawei

March 20th, 2019 1 min read

Na AFP

BRUSSELS, UBELGIJI

WAZIRI wa masuala ya nje Wang Yi, mnamo Jumatatu alikemea kile alichokitaja kuwa shtuma zisizo za kawaida na zilizokosa maadili dhidi ya kampuni ya mawasiliano ya Huawei.

Kampuni hiyo imekuwa ikishambuliwa na Amerika kuwa ni hatari kwa usalama wa mataifa ya magharibi.

Yi alidai kuwa kampuni hiyo, pamoja na nyingine za China zinanyimwa mazingira yenye ushindani sawa sokoni.

Alisema hayo alipokutana na mawaziri wa masuala ya nje wa Muungano wa Ulaya (EU) na maafisa wengine wa serikali, Jijini Brussels, Ubelgiji.

Matamshi ya waziri huyo yametolewa wakati Washington imekuwa ikihimiza wandani wake, hasa bara Uropa, kuzuia kampuni ya Huawei kushiriki biashara hasa ya kuweka miundombinu ya Intaneti ya 5G ambayo inatarajiwa kuanza kutumika, kwa sababu ya ushirikiano wa kampuni hiyo na serikali ya China.

“China inatumai kuwa nchi zote zitaunda mazingira ya haki kwa ushindani wa kampuni kutoka nchi zote. Tunachopinga ni shtuma zisizo na msingi ambazo zinashinikizwa na sababu za kisiasa na kutaka kuangusha kampuni ya nje.”