Habari Mseto

Yafichuka raia wa kigeni 35,000 wamepata kazi Wakenya wakitaabika

March 26th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

JUMLA ya raia wa kigeni 35, 413 wamepewa leseni za kufanyakazi kazi nchini katika zaidi ya sekta 10 kati ya Julai 1, 2015 na Juni 30, 2018, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ameliambia bunge la kitaifa.

Kwenye taarifa iliyowasilishwa Jumanne kwa niaba yake mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Leba Dkt Matiang’i alisema wengi wa raia hao wa kigeni wanafanya katika sekta za ujenzi wa barabara na reli, sekta utengenezaji bidha (kama vile vyuma, saruji, matofali na ushonaji nguo) ujenzi wa nyumba, uhandisi, udaktari kati ya mengine.

Kulingana na Dkt Matiang’i, wageni hao wanatekeleza kazi maalum “zinazohitaji ujuzi spesheli ambao haupatikani nchini.”

“Wengine wao pia wanafanya kazi humu nchini baada ya kutumwa na mashirika ya kigeni yenye matawi humu nchini huku wengine wakipata mwanya kwa mujibu wa kanuni za Mamlaka ya Uwekezaji Nchini (KIA) ambayo inaruhusu kila mwekezaji kuleta wafanyakazi wa kigeni,” akasema.

Dkt Matiang’i alisema kuwa baadhi ya wataalamu wa kigeni pia wamepata nafasi ya kufanya kazi humu nchini kutokana na haja ya kuwezesha mashirika ya kigeni kupenya soko la ukanda huu, hasa Kenya.

“Wengine pia huja kufanyaka nchini kwa misingi ya makubaliano ya kimataifa kama vile; Makubaliano kuhusu Soko la Pamoja la Afrika Mashariki kando na usaidizi wa Mamlaka ya Kitalii Nchini (KTB), Bodi ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali kati ya mashirika mengine,” akaileza Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Bura Ali Wario.

Waziri msaidizi katika wizara ya Dkt Matiang’i Bw Ole Ntutu aliandamana na Katibu katika Idara ya Uhamiaji Dkt Kihalangwa kufika mbele ya kamati hiyo.

Dkt Matiang’i alifafanua kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa Wakenya hawapoteza nafasi haba za ajira kwa wageni hao.

“Hatua hii tunafanya kwa kukataa maombi ya wageni ambao ujuzi na talanta zao tayari zinapatikana humu nchini. Pia tunahakikisha kuwa mashirika ya kitaalamu yanawapiga msasa wageni wanaowasilisha maombi ya kutaka wapewe lesini za kufanya kazi humu nchini,” akaeleza.

Waziri Matiang’i alitoa maelezo hayo kufuatia ombi la Kamati hiyo la Leba kutaka ielezwe kuhusu sera ya sasa inayoongozwa uajiri wa wageni humu nchini.

Hii ni kufuatia malalamishi ambayo iliwasilisha mbele yake Februari na Wakenya waliolalamika kuwa wageni hupewa kazi ambazo wao pia wanaweza kufanya, hali ambayo ambayo huchangia ongezeko la kero la ukosefu wa ajira nchini.

Kamati hiyo pia ilitaka hatua ambazo Idara ya Uhamiaji imeweka kudhibiti hali ambapo baadhi ya Wakenya huhisi kutengwa katika soko la ajira humu nchini huku wageni wakipendelewa.