Habari Mseto

Wakazi wa Thika wahamasishwa jinsi wanavyoweza kutumia mikopo kuboresha maisha

March 27th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Thika walikongamana pamoja mnamo Jumanne ili kuhamasishwa kuhusu umuhimu wa kupokea mikopo ya kufanyia biashara.

Wanawake na vijana zaidi ya 500 walikongamana mjini Thika lengo likiwa ni kuhamasishwa kuhusu Women Enterprise Fund.

Mbunge wa Thika Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina alikuwa mstari wa mbele kuwapa mwongozo jinsi ya kupokea mikopo na kujiendeleza nayo kupitia kuanzisha na kusimamia miradi.

“Unapochukua mkopo hustahili kuweka pesa hizo jinsi wanawake hufanya kile kinatajwa ni ‘Table Banking’. Cha muhimu ni kufanyia miradi tofauti ili kujiendeleza,” alisema Bw Wainaina.

Aliwatahadharisha wajiepushe na siasa zinazoendelea kushamiri hapa nchini.

“Ninawashauri kwa unyenyekevu muwachane na siasa za nchi na badala yake fanyeni hima muungane kama vikundi kujiendeleza na miradi. Hiyo tu ndiyo itafanya muwe na pesa mikononi mwenu,” alisema Bw Wainaina.

Malengo

Alivitaka vikundi vya wanawake vifanye hima kuungana pamoja na kukopa fedha za maana zitakazowafaidi kupiga hatua katika malengo yao ya kimaisha.

Kwa sasa serikali inapanga kujumuisha makundi yanayoungana katika ajenda nne kuu za serikali hasa za kubuni ajira na ujenzi wa nyumba za kadiri.

Alikipongeza kikundi cha vijana 29 kutoka kijiji cha Kiandutu ambao kwa ujasiri wao wanasafiri hadi Nyandarua kununua viazi na kupakia vyema huku wakiuzia watu mitaani.

“Wengi wao hawakosi kupata faida ya Sh 1,000 kila siku; jambo ambalo limepunguza maovu mengi mitaani kupitia hatua hiyo,” alisema Bw Wainaina.

Alisema zabuni zinazopewa wageni hasa Wachina; za ujenzi wa majumba makubwa hapa nchini, zinastahili kupewa wale walioungana kwa vikundi na wanaendesha miradi ya ujenzi.

“Kwa mfano mkiwa katika kikundi chenu cha wanawake mnaweza kununua ardhi kama ekari sita hivi na muanze ujenzi wa nyumba za watu kuishi kwa kulipa kodi. Bila shaka serikali itafanya juhudi kuwapiga jeki ili kuendelea zaidi,” alisema Bw Wainaina, na kuongeza yeye pia yuko tayari kuwapiga jeki “iwapo mtaonyesha mfano mwema.”

Alitaka vikundi hivyo viwe na maono ya kuweka fedha nyingi ambapo hata kama wana Sh1 milioni kwenye hazina yao wanaweza pewa kiasi cha Sh3 milioni kwa miradi yao.

Bw Samuel Thuo, wa kikundi cha Women Enterprise Fund, alisema vikundi vitakuwa vikipewa mikopo iwapo wataonyesha  wazi ni miradi ipi wananuia kutekeleza.

“Kutoka wakati huu mikopo itatolewa  kulingana na mambo munayofanya  kwenye vikundi. Hatutaki fedha zinazotolewa ziwe za kuweka ama kukopeshana miongoni mwenu jinsi wengi wenu mmezoea kufanya,” alisema Bw Thuo.

Aliwahimiza wawe wakianza kufanya  miradi midogo ili kujiendeleza zaidi, huku akiwaonya wale ambao hukosa kulipa ya kwamba hawatakubaliwa kupata mikopo mingine iwapo hawatakamilisha deni lao