HabariSiasa

HALI YA TAIFA: Uhuru asitasita kuhusu ufisadi

April 4th, 2019 2 min read

BENSON MATHEKA na PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta Alhamisi alisita kuchukua hatua madhubuti dhidi ya mawaziri wanaochunguzwa kwa ufisadi, alipohutubia bunge kuhusu Hali ya Taifa.

“Nimewekewa presha na watu wanasubiri kujua nitamfuta nani. Hata hivyo uchunguzi ni lazima ufanywe kwa misingi ya kisheria,” akasema.

Mawaziri kadhaa wamehojiwa kuhusiana na sakata za ufisadi wakiwemo Henry Rotich (Fedha), Mwangi Kiunjuri (Kilimo), Eugene Wamalwa (Ugatuzi) na Simon Chelugui (Maji).

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress, Musalia Mudavadi, ambaye pia alikuwa bungeni, alitofautiana na Rais, akisema maafisa wote wa serikali ambao tayari wamefika mbele ya asasi za kuchunguza ufisadi kuhojiwa wanapaswa kujiuzulu, kwani wanaaibisha Rais na Kenya kwa kuendelea kuwa afisini.

“Ikiwa wewe umekuwa mgeni wa DCI na EACC, hauoni kuwa unaaibisha serikali na Rais? Usingoje upelekwe kortini ndio utoke,” akasema Bw Mudavadi.

“Rais amesema yeye hatafuta watu lakini atasubiri waingie kortini. Hapo ndipo ninamkosoa kwa sababu yeye anasema anataka kufuata sheria. Lakini ni vigumu sana kufanya uchunguzi wa kutosha kama mtu yuko ofisini,” Bw Mudavadi alisema.

Mkurugenzi wa DPP, Noordin Haji amekuwa akilalamika kuwa watu wanaochunguzwa kwa ufisadi wakiendelea kuhudumu katika ofisi zao huwa wanaharibu ushahidi.

Alipohutubia bunge 2015, Rais aliwasimamisha kazi mawaziri kadhaa waliokuwa wakihusishwa na ufisadi, na Wakenya wengi walitarajia angefanya hivyo jana.

Rais alikiri kuwa ufisadi unahatarisha ufanisi ambao umepatikana nchini, kulemaza ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa elimu na hata utawala wa sheria.

Kwenye hotuba yake jana, Rais alisisitiza kuwa hatalegeza vita dhidi ya ufisadi: “Hatutarudi nyuma kwa sababu tunataka kuachia watoto wetu Kenya bora kuliko tuliyorithi. Hata hivyo, ni lazima nionye kuwa vita dhidi ya ufisadi vitaendelezwa kwa kufuata sheria. Ingawa vyombo vya habari vinaunga juhudi zetu inavyostahili, vitendo vyetu havitalenga kuhukumu kabla ya mtu kupatiwa nafasi ya kujitetea,” alisema.

Alisifu hatua ambazo idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na Ofisi ya Mashtaka ya Umma (DPP), zinachukua kuchunguza na kushtaki washukiwa wa ufisadi.

“Msingi wa demokrasia yetu ni utawala wa kisheria na msingi wa kufuata mfumo unaostahili ni nguzo muhimu. “Tunafaa kufuata msingi huu na kuhakikisha hatutendi haki katika sehemu moja kupitia ukiukaji wa haki katika sehemu nyingine,” alisema.

“Ningali na imani kwamba asasi zetu za uchunguzi na mashtaka zitatenda haki kupitia ushahidi na kuheshimu sheria,” aliongeza Rais Kenyatta.

“Kama vile nimewahi kusema hapo mbeleni, ninajitolea kuchukua hatua na kuondoa kutoka serikali mtu yeyote ambaye atafikishwa kortini kujibu kesi,” alisema.

Na kwa mara nyingine, Rais alinyoshea lawama Mahakama kwa kuwa kizingiti katika vita dhidi ya ufisadi, akisema Wakenya wanataka kuona watu wakifungwa jela kwa kupora mali ya umma.

Sawa na alivyosema miaka iliyotangulia, Rais Kenyatta alisema hakuna atakayesazwa kwenye vita dhidi ya ufisadi.

“Hakuna kulegeza kamba katika vita dhidi ya ufisadi. Hakuna atakayesazwa, hakuna kubadili nia. Vita dhidi ya ufisadi ni vita vya moyo wa taifa letu,” alisema.

Katika tamko lililoonekana kulenga wanaokosoa vita hivyo na kupanga kupunguza mamlaka ya DCI na DPP, Rais Kenyatta alisema anaazimia kutia nguvu idara hizo.