Michezo

Chipu yahitaji Sh25 milioni kuenda Brazil

April 12th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Kenya ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya chipukizi maarufu Chipu inahitaji Sh25 milioni kushiriki Raga ya Dunia ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 nchini Brazil mwezi Julai mwaka 2019.

Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Ijumaa, Afisa Mkuu Mtendaji Sylvia Kamau alifichua, “Bajeti ya Chipu ni zaidi ya Sh25 milioni. Fedha hizi zitatumika katika maandalizi ya Chipu, usafiri, kulipia mahali pa kulala, vyakula, dawa na marupurupu ya wachezaji pamoja na benchi la kiufundi.”

Alitangaza kwamba Chipu, ambayo inajumuisha wachezaji wengi kutoka vyuo vya mafunzo ya juu, itaanza kujitayarisha majuma mawili yajayo kujiweka tayari kwa mashindano hayo ya mataifa manane.

“Tunasalia na wiki 12 kabla ya Raga ya Dunia kwa hivyo tuna muda mchache sana wa kujiandaa. Watafanya mazoezi kwa siku tatu kwa wiki,” alisema Kamau.

Kocha Paul Odera aliongeza kwamba Chipu itafanyiwa uchunguzi wa kiafya na mazoezi ya viungo mnamo Aprili 15 kabla ya kuanza mazoezi ya uwanjani Aprili 23.

“Ni ratiba ngumu. Tulishinda raga ya Barthes Trophy kundi ‘A’ wiki moja tu iliyopita. Sasa, tunasalia na chini ya wiki 12 kabla ya kuelekea Brazil,” alisema Odera ambaye anatarajiwa kutajwa kocha mkuu wa timu ya watu wazima wakati Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) litakutana mwisho wa Aprili.

Odera alitarajiwa kutwikwa majukumu ya kunoa Kenya Simbas baada ya kipute cha Barthes jijini Nairobi, lakini sasa atasubiri hadi mwisho wa mwezi kufahamu kama atapewa kazi hiyo ama la kwa sababu majukumu yake sasa ni kuongoza Chipu kwa kipute cha Brazil kitakachofanyika Julai 9-21 mwaka 2019.

Wadhifa wa Simbas uliachwa wazi baada ya KRU kupiga kalamu Ian Snook na msaidizi wake kutoka New Zealand Murray Roulston mwezi Januari baada ya wao kushindwa kufikisha timu hiyo katika Kombe la Dunia litakaloandaliwa nchini Japan baadaye mwaka 2019.