Michezo

Euronuts, Barcelona Ladies mabingwa wa Chapa Dimba na Safaricom

April 16th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE 

BINGWA mtetezi kwenye michezo ya Chapa Dimba na Safaricom Makala ya Eneo la Kati, Euronuts, na Barcelona Ladies zimeibuka mafahali na malkia wa kipute hicho mwaka 2019 baada ya kufanya kweli katika fainali zilizopigiwa uwanjani Thika Stadium, Thika.

Timu ya wavulana ya Euronuts ya Kiambu ilihifadhi ubingwa huo ilipokomoa Lufa Graduates kwa mabao 2-1 nao wasichana wa Barcelona Ladies walitwaa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Limuru Starlets na kuzoa tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa.

Kikosi cha Euronuts kiliteremsha soka safi na kufanya wenzao kukosa ujanja baada ya Lual Mengistu kukiweka kifua mbele dakika ya sita.

Bao la pili lilifumwa na George Ndungu katika dakika ya 35 kabla ya Lufa Graduates kuzoa bao la kufuta machozi lililotingwa na Daniel Lorere dakika 30 baadaye.

Naye Florence Ngonyo aliifungia Limuru Starlets bao la pekee huku Jane Njeri wa Barcelona Ladies akitikisa wavu mara mbili.

Pia alituzwa mfungaji bora alipotinga magoli sita kwenye mechi mbili.

“Sina budi kuwapongeza wenzangu kwa kushusha mechi nzuri pia kupiga hatua kushiriki fainali za kitaifa,” Jane Njeri alisema.

Euronuts na Barcelona Ladies kila moja ilituzwa kombe, Sh200,000 na medali na pia simu yenye thamani ya Sh10,000 kwa kila mchezaji.

Tuzo kwa wachezaji walioonyesha umahiri

Kitengo cha wasichana, Jane Njeri aliibuka mfungaji bora alipocheka na wavu mara sita ndani ya mechi mbili huku tuzo hiyo ikiendea Lual Mengitsu kwa wavulana baada ya kufungia Euronuts mabao mawili.

Katika kategoria ya MVPs, waliotuzwa ni John Mutuma (wavulana) na Miriam Lutomia (wasichana).

Nao David Wainaina (Euronuts) na Eunice Alele (Barcelona) walitwaa tuzo ya mlinda lango bora kwa wavulana na wasichana mtawalia.