Habari Mseto

Mkazi wa Gatanga aliyefariki katika hali tatanishi azikwa

April 17th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE  ONGARO

FAMILIA moja katika kijiji cha Riambara, Gatanga, Kaunti ya Murang’ a, inataka haki itendeke baada ya mwana wao kuuawa.

Ilidaiwa marehemu Michael Kinuthia, aliuawa na ‘washukiwa ambao wanajulikana’ lakini hawajanaswa na polisi.

Babake marehemu Joseph Kinuthia, alisema jina la mtu anayeshukiwa kuwa ndiye alimuua marehemu linajulikana.

“Marehemu alikuwa akifanya kazi ya kibarua na mnamo siku hiyo alikuwa amepewa kazi fulani ya kufanya. Baadaye kazi hiyo ilipokosa kutekelezwa alitumiwa wahuni walioelezwa kutekeleza uovu huo,”  alisema Bw Kinuthia ambaye ndiye babake mzazi.

Waombolezaji waliohudhuria mazishi ya marehemu Michael Kinuthia wakitoa heshima zao za mwisho. Picha/ Lawrence Ongaro

Wakati wa mazishi yaliyofanyika Jumanne, Bw Kinuthia aliitaka serikali kupitia idara ya DCI kufanya uchunguzi wa kina ili kuweza kupata kiini cha kifo hicho.

“Ninachoomba serikali ni kuona ya kwamba haki imetendeka na wale waliohusika kutiwa nguvuni haraka iwezekanavyo,” alisema Kinuthia.

Majeraha

Upasuaji uliofanywa ulionyesha kuwa  marehemu alipata majeraja mabaya kichwani, miguuni, na hata kwenye mikono.

Matokeo ya ripoti ya daktari yalieleza kuwa marehemu alifariki kutokana na sumu.

Huku akiongea akiwa na huzuni tele babake marehemu alihofia pengine hilo halingetokea iwapo marehemu angeelewana na mwajiri wake kuhusu maswala ya kazi.

“Mimi naelewa ya kwamba vijana wangu aliyekuwa na umri wa miaka 39 alikuwa mtu wa amani na sioni ni kwa nini anaweza kuuawa kinyama hivyo bila sababu maalum. Mimi naomba serikali itufanyie heshima kubwa ili tujue ukweli wa mambo,” alisema Bw Kinuthia.

Alipendekeza washukiwa wa mauaji hayo wachukuliwe hatua kali bila huruma ili liwe funzo kwa watu wenye nia mbaya ya kuangamiza maisha ya watu.

Mchungaji wa wa Kanisa la PCEA, Bw John Mwaura, alisema ni makosa kukatisha maisha ya kijana mwenye bidii kama marehemu, huku akitaka haki itendwe kwa familia.

“Maisha ya mwanadamu ni muhimu ulimwenguni na sio vyema kwa maisha kupotea kiholela hivyo,” alisema Bw Mwaura, na kuongeza hata katika katiba ya nchi hairuhusu maisha ya mtu kukatishwa kiholela.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na waombolezaji wengi ambao walionyesha hasira na huzuni, huku wengi wao wakionekana kunong’onezana kwa sauti ya chini.