Chelsea, United na PSG zamhemea Coutinho

Chelsea, United na PSG zamhemea Coutinho

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

CHELSEA wamefichua nia ya kumsajili kiungo Philippe Coutinho katika juhudi za kulijaza pengo la Eden Hazard ambaye dalili zote zinaashiria kwamba huenda akayoyomea Real Madrid mwishoni mwa msimu huu.

Kwa mujibu wa gazeti la Telefoot nchini Uingereza, Chelsea huenda pia wakashawishika kuziwania huduma za fowadi Nicolas Pepe wa Lille iwapo jitihada za kumsajili Coutinho zitagonga mwamba.

Hata hivyo, itawalazimu Chelsea kutoana jasho na vikosi kadhaa maarufu vya bara Ulaya katika vita vya kupigania saini ya kiungo huyo anayemezewa pia na Manchester

Hata hivyo, Chelsea watasubiri zaidi kusajili mchezaji yeyote iwapo Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) litadumisha marufuku ya kutojishughulisha sokoni kwa minajili ya kuwania huduma za sogora yeyote.

Mbali na kuwania maarifa ya Coutinho, kocha Zinedine Zidane pia anazikeshea huduma za Paul Pogba ambaye mustakabali wake kambini mwa Man-United unaanza kuning’inia padogo uwanjani Old Trafford.

Coutinho, 26, hata hivyo, ameanika mipango ya kubanduka Barcelona mwishoni mwa msimu huu na kuelekea Old Trafford kuvalia jezi za Man-United.

Nyota huyo mzaliwa wa Brazil aliagana na Liverpool yapata miezi 14 iliyopita na kurasimisha uhamisho wake hadi Barcelona kwa kima cha Sh19 bilioni.

Kwa mujibu wa gazeti la The Mirror nchini Uingereza, Coutinho amewaeleza baadhi ya marafiki zake nchini Uingereza kuhusu mipango yake ya kurejea Uingereza kupiga soka ya kulipwa katika Ligi Kuu ya EPL.

Man-United wapo radhi kufungulia mifereji yao ya pesa na kujinasia huduma za Coutinho kwa kima cha Sh14 bilioni, pesa zitakazomweka miongoni mwa wachezaji ghali zaidi katika historia ya kipute cha EPL.

Japo ni matamanio ya Coutinho kurejea ugani Anfield kuvalia jezi za Liverpool, kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp huenda kisiwe radhi kuwania upya huduma za sogora huyo aliyejenga kuta za uadui kati ya Liverpool na Barcelona wakati akibanduka Uingereza.

Hata hivyo, habari za kutua kwake Old Trafford huenda zisipokelewe vyema na mashabiki wa Liverpool ambao ni watani wakubwa wa Man-United. Man-United kwa sasa watalazimika kutoana jasho na Chelsea na Paris Saint-Germain (PSG) ambao pia wanazihemea huduma za Coutinho usiku na mchana.

PSG wana kiu ya kulipiza kisasi dhidi ya Barcelona waliowakalia mguu wa kausha katika jitihada za kumsajili kiungo chipukizi mzawa wa Uholanzi, Frenkie De Jong. Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, PSG walipigiwa upatu wa kujitwalia huduma za Coutinho hata kabla ya Barcelona kumwahi kiungo huyo mnamo Januari 2018.

Kufikia sasa, Coutinho amewajibishwa na Barcelona katika jumla ya mechi 65 na kupachika wavuni mabao 19 pekee.

Wakati uo huo, Liverpool wanapania kumpokeza Virgil van Dijk, 27, mkataba mpya utakaomshuhudia akilipwa msha-hara wa hadi Sh28 milioni kwa wiki ili kuwazima Barcelona na Real wanaomsaka beki huyo matata mzawa wa Uholanzi.

You can share this post!

Patashika leo K’Ogalo wakiwashukia Bandari katika KPL

KAZI BADO: Tottenham Hotspur kualika Brighton huku Saints...

adminleo