Habari Mseto

Gathoni Wa Muchomba awakosoa viongozi ambao kila wakiamka ni '2022'

April 24th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI nchini wamehimizwa kuzingatia zaidi maswala ya maendeleo badala ya kupiga siasa.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu katika Bunge la Kitaifa, Bi Gathoni Wa Muchomba, amewakashifu viongozi ambao wameleweshwa na siasa za mwaka wa 2022.

“Hawa viongozi ambao wanazunguka kila sehemu ya nchi wakijitafutia umaarufu na tayari kwa uchaguzi wa mwaka wa 2022 wanakosea wananchi na ni vyema wajisahili na wazinduke walipo,” alisema Bi Muchomba.

Gathoni Wa Muchomba akijumuika na wakazi wa Kiambu ambao walinufaika na basari. Picha/ Lawrence Ongaro

Aliyasema hayo mnamo Jumanne alipotoa hundi za pesa za basari kwa vikundi tofauti.

Zaidi ya Sh4 milioni ziliwasilishwa kwa watoto na wazazi wenye ulemavu. Wengine walionufaika ni watoto wasio na walezi wao na mayatima.

Vijana wapatao 300 pia walinufaika na masomo ya kiufundi ambapo watajumuika pamoja na wengine 1,000 ambao walikuwa wamejiunga na masomo hayo hapo awali.

Bi Muchomba aliwasuta viongozi wanaokashifu salamu za maridhiano baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Ushirikiano wa wawili hao ni muhimu kwa nchi na yeyote anayepinga hana zuri la kuwazia wananchi. Kwa hivyo, ni vyema kuukumbatia kwa kauli mmoja,”  alisema Bi Muchomba.

Alisema jambo muhimu ambalo Rais Kenyatta alifanya baada ya uchaguzi wa 2017 ni kujitolea na kutafuta njia mwafaka ya kuleta Wakenya pamoja na ndiposa alimtafuta mshindani wake – Bw Odinga.

Aliwakosoa viongozi wachache ambao wanazunguka Kaunti ya Kiambu wakisema wanajenga barabara.

Alifafanua kuwa baadhi ya barabara zinazojengwa Kiambu zimefadhiliwa na serikali kuu wala sio ya Kaunti.

Aliwashauri viongozi wa kutoka Mlima Kenya ambao ‘wamemkosea heshima’ Rais Kenyatta wajirekebishe na kutendea wananchi kazi.

Aliwahimiza viongozi wajitume na kusisitiza ajenda nne kuu za serikali ili wananchi wanufaike baada ya miaka mitatu inayokuja.

Aliwafahamisha viongozi wafahamu kuwa kiongozi wa Jubilee ni Rais na kwa hivyo viongozi waache kuzungumzia chama hicho bali wajishughulishe na maendeleo kwa wananchi.