Habari Mseto

Uchimbaji mawe eneo la Kiboko sasa ni marufuku

May 7th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

ENEO la uchimbaji mawe la Kiboko (UTI), Thika, limefungwa mara moja kwa sababu za usalama kiafya.

Afisa msimamizi wa Kaunti ndogo ya Thika Bw Christopher Wanjau alisema Jumatatu kwamba wakazi wa eneo la Kiboko wamelalamika ya kwamba katika eneo hilo kumekuwa kukilipuliwa baruti kila mara huku nyumba zao zikipata nyufa.

Bw Wanjau alifanya ziara ya ghafla na maafisa wake wakuu ili kujionea mwenyewe jinsi kazi inavyoendeshwa katika eneo hilo.

“Tayari nimefika mahali hapa na nimejionea madhara yanayoweza kupatikana. Kwa hivyo, afisi ya Kaunti ya Kiambu imeonelea kusitisha uchimbaji wa mawe na biashara nyingine za kununua mawe hayo,” alisema Bw Wanjau.

Alipoandamana na waandishi wa habari na askari wa kaunti walipata wafanyakazi mahala hapo wakiendelea kuchimba mawe na wengine kuyapakia kwenye malori yaliyofika hapo.

“Hatuwezi kukubali biashara ya kuchimba mawe iendelee hapa kwa sababu hapa ni karibu na makazi ya watu, na pia kuna shule ya upili na ya msingi karibu,” alisema Bw Wanjau.

Awatahadharisha

Akiwahutubia wafanyakazi wa hapo, afisa huyo aliwatahadharisha kuhusu madhara  yanayoweza  wapata iwapo wataendelea  kufanya kazi mahali hapo.

Alisema kwanza ni hatari kwa usalama wao kwa sababu  hata vumbi inayotokea mle ndani ni hatari kwa afya ya binadamu. Pia mtu anaweza kuangukiwa na jiwe kutoka juu ya mwamba na kusababisha kifo.

“Kwa hivyo, sisi tumefika hapa kuwapa mawaidha na kuwashauri ya kwamba kazi ya hapa imesitishwa mara moja. Lakini kwa sababu tunaelewa hali ya maisha jinsi ilivyo tunawapa muda wa siku saba kukamilisha biashara yoyote au zozote mlizokuwa mmezipanga,” alisema Bw Wanjau, na kuongeza iwapo mtu atakayepatikana akiendesha biashara yake eneo hilo baada ya muda huo wa siku saba, bila shaka atajipata mikononi mwa sheria.

Bw Raphael Njehe, afisa msimamizi wa Kaunti ndogo ya Thika, aliwajulisha wafanyakazi hao kufuata maagizo hayo kwa makini sana kwa manufaa ya  maisha yao wenyewe.

“Hatungetaka kuwadhulumu kwa vyovyote vile. Tumekuja tu kutoa ilani kwenu ili mfuate maagizo yetu,” alisema Bw Njehe, na kuongeza yeyote atakayekiuka sheria hiyo atajilaumu mwenyewe.

Mfanyakazi mmoja ambaye anaponda mawe kugeuka kokoto, Bi Susan Wanjiku Njuguna, anasema maisha yao ya baadaye yataathirika kwa sababu wana watoto nyumbani wanaowategemea kwa vyovyote vile.

“Sasa nyinyi wakubwa mnataka twende wapi iwapo tutakosa kufika mahali petu pa kutafutia riziki? Hapa ndipo mahali tumezoea kuja kutafuta unga kila siku. Hebu tupatieni njia mwafaka ya kujitafutia unga kwa watoto wetu,” aliteta kwa hasira Bi Wanjiku.

Hata hivyo wafanyakazi hao waliarifiwa wafuate maagizo hayo kabla ya maslahi yao kushughulikiwa hapo baadaye.

 

Afisa msimamizi wa kaunti ndogo ya Thika, Bw Christopher Wanjau (katikati) awahutubia wafanyakazi katika eneo la uchimbaji mawe lililoko Kiboko, mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro