Michezo

Shujaa yafufua matumaini ya kusalia Raga ya Dunia kwa kulaza Samoa

May 25th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Kenya imefufua matumaini ya kuingia robo-fainali kuu kwa mara yake ya kwanza kwenye Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 baada ya kuduwaza Samoa pembamba 21-20 Jumamosi katika mechi yake ya pili ya Kundi B jijini London nchini Uingereza.

Shujaa, ambayo pia ilikuwa imechapwa na Samoa katika mechi mbili zilizopita, ililipiza kupitia kwa miguso mitatu kutoka kwa chipukizi Vincent Onyala.

Chipukizi mwingine Johnstone Olindi alipachika mikwaju ya miguso hiyo.

Vijana wa kocha Paul Murunga walijipata chini alama 10-0 baada ya Samoa kufunga miguso bila mikwaju kupitia kwa Melani Matavao na Tomasi Alosio.

Onyala alipunguza mwanya huo hadi alama tano kupitia mguso baada ya kupokea pasi murwa kutoka kwa Olindi dakika ya saba.

Olindi alipachika mkwaju wa mguso huu.

Kabla ya ya wino kukauka, Onyala alipata mguso wake wa pili baada ya Andrew Amonde kukaba mchezaji wa Samoa.

Olindi hakukosea kuongeza mkwaju, huku Kenya ikienda mapumzikoni alama tatu nyuma, 10-7.

Mambo yalionekana kuwa mabaya kwa Shujaa pale Laaloi Leilua alianza kipindi cha pili kwa kufungia Samoa mguso uliowaweka mbele 15-7.

Kenya ilifanya makosa mengi katika kipindi hiki cha pili, lakini bidi yake ikaifanya kupata mguso mwingine kutoka kwa Onyala na mkwaju kutoka kwa Olindi.

Ingawa Samoa ilifunga ukurasa wa alama kupitia mguso wa Alamanda Motuga, haikuweza kupiku Kenya kwa sababu ilikosa mkwaju wake.

Kenya sasa itafahamu hatima yake ya kuingia mduara wa nane-bora mjini London itakapokutana na Ufaransa saa kumi na mbili na dakika 26 hii leo Jumamosi.

Ushindi utahakikishia Kenya nafasi katika robo-fainali na kupunguza presha inayoikabili ya kukodolea macho kutemwa.