Kimataifa

Serikali ya Tshisekedi kudhibitiwa na Kabila

May 30th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

KINSHASA, DRC

ALIYEKUWA Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Joseph Kabila atakuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya Rais wa sasa Felix Tshisekedi kwani asilimia 60 ya watu watakaoteuliwa katika baraza jipya la mawaziri watakuwa wandani wake.

Kulingana na makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo yaliyofanyika katika mji wa Kisantu, chama cha Bw Kabila cha Common Front for the Congo (FCC) kimetengewa asilimia 60 ya nafasi katika baraza hilo huku muungano wa vyama vilivyomuunga mkono Rais Tshisekedi katika uchaguzi mkuu vitachukua asilimia 20 ya nafasi.

Muungano huo ni CACH.

Wiki jana Rais Tshisekedi alimteua Bw Ilunga Sylvester ambaye ni mwandani wa Bw Kabila kuwa Waziri Mkuu, ishara kwamba Rais huyo wa zamani bado atakuwa na ushawishi mkubwa katika utawala wa sasa.

Kituo cha Redio OKAPI kiliripoti kuwa baraza hilo la mawaziri linakuwa na mawaziri 39 pamoja na mawaziri wasaidizi 12.

Bw Kabila kama kiongozi wa chama cha FCC atapendekeza moja kwa moja majina ya watu watano katika baraza la mawaziri, idadi sawa na ile Rais Tshisekedi atapendekeza.

Hii ina maana kuwa katika orodha ya mwisho ya mawaziri Rais Tshisekedi atakuwa na asilimia 30 pekee na mawaziri huku wengine wakiegemea upande wa Kabila.

Miezi minne baada ya kuapishwa kwake, Rais Tshisekedi amekuwa akiongoza bila Waziri Mkuu ambaye kwa mujibu wa Katiba ya DRC ndiye anapaswa kuongoza baraza la mawaziri.

Wadadisi wanasema Rais Tshisekedi hawezi kuongoza bila usaidizi na mwelekeo kutoka kwa Bw Kabila ambaye chama chake, FCC, kina wabunge 337 katika bunge lenye jumla ya wabunge 500.

Na chama cha FCC pia kina magavana 23 kati ya 24 na maseneta 91 kati ya 100 .

Kwa upande mwingine muungano wa vyama vilivyomuunga mkono Tshisekedi, CACH, una jumla ya wabunge 50.

Ushawishi

Sababu moja iliyosababisha kucheleweshwa kwa uteuzi wa baraza la mawaziri ilikuwa ni hofu kwamba Kabila bado ana ushawishi mkubwa bungeni.

Hiyo ina maana kuwa chama cha FCC kinaweza kumwondoa mamlakani Rais kikitaka.

Hali hii imekipa chama hicho nguvu kushawishi teuzi serikalini na hata uwezo wa kubadilisha Katiba.

Rais Tshisekedi aliingia mamlakani Januari 2019 na kuahidi kupambana vikali na zimwi la ufisadi na kuimarisha rekodi ya DRC kulinda haki za binadamu.

Hata hivyo, imedhihirika wazi kuwa ufanisi wake utategemea pakubwa uungwaji mkono atakaopata kutoka kwa Rais (Mstaafu) Kabila.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga