Habari

Waliosajiliwa Huduma Namba ni 37.7 milioni – Uhuru

June 1st, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

WAKENYA 37.7 milioni ndio waliosajiliwa kwa Huduma Namba kufikia sasa, Rais Uhuru Kenyatta amesema.

Hata hivyo, hilo limekosa kutimiza lengo la serikali la kuwasajili Wakenya 45 milioni ilivyokusudia.

Akihutubu Jumamosi kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya Madaraka, Rais Kenyatta alisisitiza kuhusu umuhimu wa namba hiyo, akisema kuwa itawarahisishia Wakenya mzigo wa kubeba stakabadhi nyingi wanapopokea huduma za serikali.

Muda wa Wakenya kujisajili kwa namba hiyo uliisha mnamo Mei 18 na waliokosa kusajiliwa wanapaswa kufika kwa machifu kushughulikiwa.

“Namba hii itakuwa muhimu kwa Wakenya, kwani itawapa nafasi ya kuhudumiwa na serikali kwa urahisi,” alisema rais.

Maswala mengine aliyoyapa kipao mbele katika hotuba yake ni ukuaji wa uchumi, akisema kuwa kufikia sasa, uchumi wa Kenya umestawi kwa asilimia 6.3

Hali ngumu

Hii ni licha ya hali ngumu ya uchumi kushuhudiwa katika sehemu mbalimbali duniani.

Rais vilevile alisisitiza kuwa serikai yake itaendelea kuwekeza katika Mpango wa Kutoa Afya kwa Wote, ili kuhakikisha kuwa hakuna Mkenya anayekosa matibabu kwa msingi wa gharama yake.

Hivyo, alisema kuwa Serikali Kuu itapanua ushirikiano wake na serikali za kaunti, ili kuhakikisha mpango huo umefaulu bila matatizo