Makala

UCHAMBUZI: Handisheki yakanganya viongozi wa ODM

June 7th, 2019 4 min read

Na CHARLES WASONGA

MIKINZANO ya kimawazo inayodhihirika ndani ya ODM katika siku za hivi karibuni kuhusiana na baadhi ya sera za serikali imeonyesha kuwa siri za muafaka kati ya kiongozi wake Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta zinakanganya viongozi wake.

Tangu Machi 9, 2018, wawili hao walipotia saini muafaka huo – maarufu kama handisheki – ambao ulileta utulivu katika ulingo wa siasa nchini, baadhi ya wabunge wa ODM wamekuwa wakionekana wakipinga baadhi ya maongozi ya serikali.

Miongoni mwao ni mwenyekiti John Mbadi na Seneta wa Siaya James Orengo, ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Odinga.

Kulingana na wadadisi, wabunge hao wameonekana kuchanganyikiwa kuhusu iwapo handisheki ilimaanisha kuwa wataunga mkono mipango, sera na maongozi yote ya serikali ndani na nje ya bunge.

Vilevile, huenda hawafahamu iwapo baada ya handisheki wanapaswa kuendelea kuvumisha azma ya Bw Odinga ya kuingia Ikulu au wanapaswa kusubiri hadi miezi kabla ya uchaguzi mkuu.

Na baadhi yao wamekanganyika kiasi kwamba hawafahamu kama kiongozi wao bado atawania urais mwaka 2022 au ataunga mkono mgombeaji mwingine kutoka ndani ya ODM, chama kingine au muungano wa kisiasa ambao huenda ukabuniwa.

Kutoa nafasi

Isitoshe, wabunge hao wanaonekana kutofahamu kama muafaka huo ulifaa kutoa nafasi kuandaliwe kura ya maamuzi ili kubadili mfumo wa uongozi kwa kubuniwa wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka.

Hali hii ya kukanyanganyikiwa kwa wabunge wa ODM na maafisa wake, ilidhihirika hivi majuzi pale Mbw Mbadi na Orengo walipinga uzinduzi wa noti mpya.

Walidai kuwa uwepo wa picha ya sanamu ya mwanzilishi wa taifa hili Mzee Jomo Kenyatta katika noti hizo mpya ni kinyume cha Katiba ambayo hairuhusu sarafu za Kenya kuwa na picha ya mtu yeyote.

Katibu Mkuu Edwin Sifuna pia alipinga noti hizo kwa misingi iyo hiyo.

Lakini msimamo huo ulipingwa vikali na wabunge wenzao Mbw Junet Mohammed (Suna Mashariki), T. J Kajwang’ (Ruaraka), Samuel Atandi (Alego Usonga) na Opiyo Wandayi (Ugunja).

Kiranja

Bw Mohammed ambaye pia ni kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa alitaja suala hilo la uwepo wa picha ya Mzee Kenyatta kwenye noti kama “lisilo na maana”.

“Sisi tunaunga mkono noti mpya. Madai ya Mbadi na Orengo na wengineo kwamba noti hizo zinakiuka Katiba ni yao kama watu binafsi na sio ya chama chetu cha ODM. Kwa hivyo lalama zao hazina maana yoyote,” akasema.

Lakini siku mbili baadaye Bw Mbadi, ambaye ni kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa alibadili msimamo huo na kusema kuunga mkono noti.

Kati kile alichodai ni “msimamo halisi wa chama” Mbunge huyo wa Suba Kusini aliishauri serikali kuhakikisha kuwa noti zitakachapishwa siku zijazo haziwekwe picha za mtu yeyote. Naye Bw Orengo, ambaye pia ni kiongozi wa wachache katika Seneti aliamua kukimya.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Profesa Macharia Munene anasema hatua ya vigogo hao wa ODM kubadili msimamo kuhusu uhalali wa noti hizo mpya kulichangiwa na kiongozi wao Bw Odinga.

“Ni wazi kuwa “Baba” aliwaamuru wabunge hao kuunga mkono sarafu hizo mpya kwa ili kusionekane kwamba chama kinachukua msimamo kinzani na ule wa serikali ya Jubilee katika kipindi hiki cha handisheki,” anasema.

“Lakini ni muhimu kuzingatia kwamba taswira hii inachangiwa na hali kwamba wabunge hawa hawaelewi hasa siri fiche ndani ya handisheki. Hawajui kama bado wanafaa kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kuhoji utendakazi wa serikali kama wabunge wa upinzani au wanafaa kuunga mkono sera na maongozi yote ya Jubilee.

“Ni wazi kuwa hawajapa ufafanuzi huu kutoka kwa Bw Odinga. Hii ndio maana hata majuzi walionekana kutoa matakaa ya Rais na kiongozi wao kuhusu kura ya maamuzi wakisema handisheki haitakuwa na maana yoyote ikiwa Katiba haitafanyiwa mabadiliko,” anasema Profesa Munene ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha USIU.

Na huku akionekana kulandana kifikra na Profesa Munene kuhusu suala hilo wakili James Mwamu anamshauri Bw Odinga kuandaa kikao na wabunge na viongozi wakuu wa ODM ili awape ufahamu kuhusu dhima kuu ya handisheki.

“Hii ni kwa sababu misimamo ya kinzani inayochukuliwa na wabunge wa ODM kuhusu sera za serikali ya Jubilee inaonyesha wazi kwamba kuna maafikiano fulani kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta ambayo hawajuzwa,” anasema.

Itakumbukwa kuwa wiki chache baada ya Machi 9 Bw Mbadi aliwasilisha hoja maalum katika bunge la kitaifa akisema ODM imekubaliana kwa kauli moja kuunga mkono ajenda za serikali ya Jubilee ndani na nje ya bunge.

Alitoa mfano, wa vita dhidi ya ufisadi ambayo ni mojawapo ya masuala tisa ambayo Rais Kenyatta na Odinga walikubaliana kuendeleza kupitia handisheki katika jitihada zao za kupalilia umoja na maridhiano ya kitaifa.

Hata hivyo, Bw Mbadi alifafanua kuwa wabunge wa chama hicho wataendelea kutekeleza majukumu yao kama wabunge wa upinzani kwa kuhoji maovu yanayoendelezwa na maafisa wa serikali.

Lakini wabunge wa vyama tanzu katika NASA kama vile Wiper, ANC na Ford Kenya walifasiri kauli hiyo ya Mbadi kumaanisha kuwa ODM kimehama upinzani na kujiunga na mrengo wa serikali bungeni.

Lakini licha ya Mbadi kudai kuwa “tutaunga serikali huku tukiendelea kuwa upinzani” Rais Kenyatta alipozuru Kisumu Desemba 2018 alitangaza kuwa Bw Odinga “yuko ndani ya serikali”.

Na akiongea katika mkutano wa kujadili maendeleo katika nyanja ya ujenzi wa miundombinu barani Afrika katika ukumbi wa Bomas, Nairobi, Rais Kenyatta alifichua kuwa yeye hushauriana na Bw Odinga kila mara kuhusiana na masuala ya kuendesha serikali.

Isitoshe, mawaziri wa serikali wamekuwa wakimtembelea Bw Odinga katika afisi zake zilizoko jumba la Capitol Hill, Nairobi kwa mashauriano kuhusu masuala mbalimbali ya serikali.

Hii, kulingana na Profesa Munene, imesababisha Bw Odinga kuonekana kuwa sehemu ya serikali wala sio kiongozi wa upinzani kama alivyotambuliwa kabla ya handisheki.

“Huenda siri ambayo akina Mbadi, Orengo, Sifuna na wengine hawajaelewa ni kwamba handisheki ilimweka kiongozi wao katika kitovu cha Serikali ya Jubilee kiasi kwamba hawezi kuipinga kwa njia yoyote,” anasema.