Habari Mseto

Wakazi wa Mataara wataka serikali ya kaunti iwajengee soko jipya

June 12th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa eneo la Mataara, Gatundu Kaskazini wanalalamikia soko lao lililo katika hali mbovu.

Jumanne, wanahabari walizuru soko hilo na kujionea hali halisi.

Wakazi hao wanadai ya kwamba kwa muda mrefu wamekosa pahala pazuri pa kuuzia bidhaa zao na wangetaka serikali ya Kaunti ya Kiambu “ifanye jambo”.

Bw James Kimani ambaye ni mzee wa kijiji anasema viongozi wao “kwa hakika wanastahili kupewa lawama.”

“Tangu tuwachague uongozini walipotea kabisa hata hawatutembelei kujua matakwa yetu. Huu sio wakati wa kupiga siasa bali ni wakati wa kuchapa kazi inayomfaa mwananchi,” alisema Bw Kimani.

Alisema kila mara kukinyesha mvua, soko hilo huwa kama zizi la ng’ombe hata hakuna yeyote hutamani kupeleka bidhaa zake pale.

Naye Bw Michael Njoroge ambaye ni mfanyabiashara katika kituo hicho cha Mataara anasema hata barabara inayoingia eneo hilo ni mbovu ambapo magari mengi hukosa kufika katika soko hilo.

“Wakati kama huu wa mvua sisi wafanyabiashara tunapata shida kubwa kabisa. Magari yanayoleta bidhaa za duka yanatoza ada ya juu ya usafirishaji kabla ya kupakua mizigo yetu,” alisema Bw Njoroge.

Alisema viongozi wao wanadai kuwa hakuna fedha zilizotengwa kwa kukarabati barabara na soko hilo la mataara.

Bi Mary Muthoni, ambaye ni muuzaji wa mboga, matunda na ndizi, kwenye kibanda chake katika kituo hicho anasema mambo ni magumu kwa wanaouza bidhaa aina ya chakula.

Bi Mary Muthoni akiwa sokoni. Picha/ Lawrence Ongaro

“Wakati kama huu wa mvua hakuna yeyote anayetaka kuingia katika soko hili. Matope ni mengi ajabu ambapo bila kuvalia viatu vya mvua vya matopeni huwezi kuingia ndani ya soko hili,” alisema Bi Muthoni.

Aliwataka viongozi wao wajitokeze na kuwatumikia wananchi bila kujihusisha sana na maswala ya siasa za mwaka wa 2022.

Baada ya wanahabari kuzuru soko hilo la Mataara, walipata eneo lote limejaa matope huku wauzaji wa vyakula wakijibana nje ya soko hilo kando ya matope wakiendesha biashara yao.

“Sisi kama wakazi wa hapa, tunataka viongozi wetu watukumbuke ili kuturekebishia soko letu. Zile shida tulizo nazo ni tele hapa kwetu,” alisema Bi Grace Wambui ambaye huuza nyanya, mboga na ndizi katika soko hilo.