Habari

Jaguar, Kobia wafikishwa mahakamani

June 27th, 2019 1 min read

BY MAUREEN KAKAH

MBUNGE wa Starehe, Charles Njagua ambaye ni maarufu kwa jina la utani Jaguar na mfanyabiashara Paul Kobia wamefikishwa mahakamani Alhamisi jijini Nairobi.

Jaguar alipelekwa Jumatano katika kituo cha polisi cha Nairobi Area kuandikisha taarifa baada ya kutoa matamshi yanayochukuliwa na ya kueneza chuki dhidi ya raia wa kigeni wanaofanya biashara nchini Kenya; hasa wala wa Tanzania aliotaka wafurushwe.

Wapelelezi nje ya majengo ya bunge walimwingiza katika gari lenye nambari za usajili za taifa la Sudan Kusini kabla ya kwenda kumhoji.

“Anazuiliwa (Jaguar) kama mshukiwa wa matamshi ya chuki na uchochezi na kuvuruga amani,” sehemu ya chapisho kwenye ukurasa wa Twitter wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ilisoma.

Matamshi ya mbunge huyo yamesababisha patashika hasa katika uhusiano wa kidiplomasia baina ya Kenya na Tanzania.

Msemaji wa serikali Cyrus Oguna, alisema matamshi ya Jaguar katu  hayaendani na msimamo wa serikali ya Kenya.

Naye Bw Kobia alikuwa na siku ndefu Kitengo cha Makosa Makubwa kilikita kambi Jumatano katika makazi yake yaliyoko Riverside Drive kuhusu sakata ya dhahabu feki iliyonuiwa kusafirishwa hadi Dubai.

Kobia na watu wengine 13 walilala korokoroni baada ya kukamatwa Jumatano. Alikamatwa pamoja na Simeon Wanaina, Paul Gichuhi, Benjamin Mutisya, Patrick Mweu, Samson Kibet, Faith Kioko na Joyce Wenani.

Wengine ni Miriam Nyambura, Consolata Thirindi, James Masai, Doreen Kathambi, Tanya Yvonne Goes na Gabriel Ndururi Murage.

Kukamatwa kwao kunakuja mara baada ya Dubai kulalama kwa kupunjwa Sh170 milioni kuhusiana na biashara ya kilo 50 za dhahabu.

Maafisa wa polisi walitwaa vijiwe saba vinavyoshukiwa kuwa ni dhahabu, magari sita, stempu ya mbao ya Banki Kuu ya Kenya, kifaa cha kupima madini, kifaa cha kuyeyusha na kuchanganya madini, mashine ya kuhesabu fedha, mashine ya ETR, stempu kadhaa na bidhaa kadhaa ambazo yumkini ni feki.