Michezo

Brazil yaliza Paraguay na kufuzu kwa 4-bora

June 29th, 2019 2 min read

PORTO ALLEGRE, Brazil

GABRIEL Jesus alipachika penalti ya ushindi, huku Brazil ikifaulu kufuta nuksi kwa kuwachapa Paraguay na kutinga nusu-fainali ya kabumbu ya Copa America, usiku wa kuamkia Ijumaa.

Mara mbili mwaka 2011 na 2015 Paraguay ilizima Brazil katika robo-fainali kupitia mikwaju ya penalti katika kombe hili la mataifa ya Amerika ya Kusini.

Willian alikaribia kufungia Brazil katika muda wa kawaida alipogonga mlingoti, huku Paraguay ikifaulu kulazimisha 0-0 kwa zaidi ya dakika 40 baada ya Fabian Balbuena kulishwa kadi nyekundu kwa kumchezea Roberto Firmino vibaya.

Kabla ya mchuano huo, vyombo vya habari nchini Brazil vilihofia kuwa timu hiyo ingepoteza tena katika upigaji penalti vikikumbusha uchungu iliopitia nchini Argentina mwaka 2011 na Chile mwaka 2015 wakati Paraguay ilipolazimisha sare katika muda wa kawaida kabla ya kutamba kupitia penalti.

Mambo yalikuwa tofauti jana pale kipa wa Brazil, Alisson alipopangua penalti ya Paraguay ya ufunguzi kutoka kwa Gustavo Gomez uwanjani Gremio Arena.

Ingawa Firmino pia ‘aliuza’ penalti yake, Derlis Gonzalez alipopiga mlingoti na kumpa Jesus fursa ya kurekebisha kosa la kupoteza penalti katika mechi iliyopita, kwa kufunga penalti ya ushindi.

Wenyeji Brazil sasa wanasubiri mshindi kati ya mahasimu wa tangu jadi Argentina ama Venezuela katika nusu-fainali itakayosakatwa Jumanne mjini Belo Horizonte.

Brazil ilionyesha dalili ya kufanya vyema kipenga cha kuanza cha mechi kilipopulizwa, ikimegeana pasi murwa katika dakika ya nne.

Everton Cebolinha alipiga krosi safi kutoka wingi ya kushoto iliyompata Dani Alves nje ya kisanduku kabla ya kumpokeza Firmino ambaye shuti lake hafifu halikumsumbua kipa Roberto Fernandez.

Sifa ya mshambuliaji wa Gremio, Everton ilionekana katika uwanja wake wa nyumbani pale mashabiki walipomshangilia kila alipogusa mpira.

Hata hivyo, mechi ilichukua mwelekeo uliotarajiwa haraka, huku Brazil ikimiliki mpira na kupiga pasi zisizohesabika.

Paraguay ilisimama imara na kuonekana kusubiri kujibu mashambulizi kwa kasi.

Brazil ilikosa kukamilisha nafasi zake na hata wakati Philippe Coutinho alipomegea Firmino mpira mzuri nyuma ya walinzi wa Paraguay baada ya kosa la Richard Sanchez, mshambuliaji huyo wa Liverpool alizidiwa nguvu akiwa na mpira.

Golikipa aokoa

Nafasi nzuri ya Paraguay katika dakika 15 za kwanza iliangukia Hernan Perez aliyempata Gonzalez akiwa peke yake karibu na mlingoti, lakini kipa Alisson alikuwa macho kuokoa.

Baada ya mechi, kocha wa Brazil, Tite alilalamika kuhusu hali ya uwanja wa Gremio.

Alisema, “Wachezaji wote waliniomba nilalamikie uwanja mbovu. Inashangaza kuwa mechi za mashindano makubwa kama haya zinasakatwa katika uwanja mbovu kama huu.”

Venezuela na Argentina ziliratibiwa kupepetana jana usiku katika robo-fainali ya pili.

Colombia na mabingwa watetezi Chile watalimana leo katika robo-fainali ya tatu mapema leo kabla ya Uruguay na Peru kukabana koo leo usiku.