Michezo

SOKA MASHINANI: Kiranga United FC

July 2nd, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KLABU ya soka ya Kiranga United FC imejitokeza kama mojawapo ya timu hodari katika kijiji cha Muruka, eneo la Kandara katika Kaunti ya Murang’a.

Hata hivyo, Kocha wa Klabu hiyo Samuel Nyoike, amekuwa mstari wa mbele kuiweka timu hiyo kileleni kwa lengo la kutambulika katika Kaunti nzima ya Murang’a.

Kwa muda wa miaka minne sasa timu hiyo imekuwa ikiwika katika eneo la Kandara, lakini mara nyingi wameshiriki mechi za kuwania mataji na za kirafiki.

Kocha Nyoike anasema hata ingawa bado hawajafanikiwa kushiriki katika Ligi ya Kaunti ya Murang’a, ukweli ni kwamba wanazidi kutamba katika mechi zao za mitaani hasa za kirafiki na za mataji.

“Vijana hawa wanayo bidii ya mchwa na wanastahili kupokea usaidizi kutoka kwa Kaunti ya Murang’a na wadhamini ili kukuza vipaji vyao,” anasema Nyoike.

Timu hiyo ya Kiranga United imekuwa ikishiriki katika mechi za kuwania taji la John Mungai Cup, ambapo timu 14 za wanaume zinashiriki, huku tano pia zikishiriki kwa upande wa wa kina dada.

Katika mechi zilizochezwa hivi majuzi, Kiranga United iliikomoa Kivunga FC kwa mabao 2-1.

Vijana hao wepesi walitoka sare na Spurs FC kwa kulimana 1-1.

Zamani kidogo, waliichabanga Nguthuru 1-0. Halafu waliweza pia kushinda Muruka United kwa mabao 2-1.

“Licha ya changamoto za hapa na pale, sisi kama waanzilishi wa klabu hii yenye vipaji, nia yetu kwa sasa ni kuona ya kwamba tunajiandaa vyema ili msimu ujao wa 2020 tuwe tumejiweka tayari kwa Ligi ya Kaunti ya Murang’a,” alisema Nyoike na kuongeza anatarajia kuwatafuta pia vijana chipukizi wenye umri mdogo wa kati ya miaka 16 hadi 22 ili kuwa tayari kwa lolote lile.

Utovu wa nidhamu

Anaongeza kuwa kwa muda mrefu sasa visa vya utovu wa nidhamu vimepungua kutokana na vijana wengi kutopata muda wa kujiunga na makundi mabaya.

Kando na hayo, wanaomba Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF) tawi la Aberdare, liinue kiwango cha kandanda ili timu za vijijini zipate mwamko wa kushabikiwa na kudhaminiwa kama timu zingine za maeneo mengine.

Kadhalika kocha Nyoike amejitolea mhanga kutumia muda wake mwingi kuzungumza na wachezaji hao kuhusu maswala mbalimbali ikiwemo maisha ya sasa ili kuwasaidia kujiepusha na matendo maovu.

Anatoa mwito kwa maafisa wanaopewa majukumu ya kukuza spoti wafanye hima kwa kujituma na kuona ya kwamba wametekeleza wajibu wao ili kuinua talanta ya vijana.