300 wapewa vyeti vya uendeshaji boti

300 wapewa vyeti vya uendeshaji boti

NA KALUME KAZUNGU

MANAHODHA 300 kutoka Lamu wamepokezwa vyeti maalum baada ya kufuzu mafundisho ya uendeshaji mashua na boti yaliyoandaliwa na Bodi ya Udhibiti wa Vyombo vya Baharini nchini (KMA).

Hafla hiyo iliandaliwa kwenye ukumbi wa Lamu Fort na kuhudhuriwa na maafisa wakuu wa KMA, ikiwemo Mkurugenzi Mkuu, Robert Njue na Mwenyekiti wa Mamlaka hiyo, Geoffrey Mwango.

Akihutubu kwenye hafla hiyo, Bw Njue alisema lengo kuu la mpango huo ni kupiga jeki usalama wa usafiri kwenye Bahari Hindi, kaunti ya Lamu na Kenya kwa jumla.

Manahodha hao 300 walihitimu mafunzo ya kuendesha vyombo vya Baharini yaliyotekelezwa na KMA mnamo Mwezi Mei mwaka huu.

Bw Njue alisema mbali na kudhibiti usalama wa usafiri wa baharini, azma nyingine ya kuwapokeza mafunzo na vyeti manahodha nchini ni katika harakati za kuondoa vyeti vilivyotolewa zamani kwa manahodha kutoka kwa Mamlaka ya Bandari nchini (KPA) na badala yake kuwapa vyeti vya kisasa vinavyotambuliwa kisheria kutoka KMA.

Bw Njue alisema mbali na Lamu, KMA pia imekuwa ikitekeleza shughuliza mafunzo na kuwapokeza vyeti mabaharia kwenye kaunti za Kwale, Mombasa na pia Ziwa Viktoria, kaunti ya Kisumu.

Aliwataka manahodha kote nchini kushirikiana ili kufaulisha mpango huo ambao pia unalenga kuwapa nafasi mabaharia kuajiriwa kuendesha vyombo vya baharini kote nchini na kimataifa.

“Tunafurahia kwamba leo tunapokeza manahodha 300 waliofuzu mafunzoyaliyotolewa na KMA hapa Lamu. Vyeti hivi vinatolewa wakati mwafaka ambapo bandari ya Lamu (Lapsset) imeanza shughuli zake. Mnaweza kutumia vyeti hivi kutafuta ajira Lapsset na sehemu zingine nchini na kimataifa. Vyeti hivi ni vya kisasa na vinavyotambuliwa kisheria,” akasema Bw Njue.

Mwenyekiti wa KMA, Geoffrey Mwango aliwataka manahodha kutilia maanani usajili wa vyombo vyao wanavyotumia kubeba abiria baharini ili kupiga jeki zaidi usalama na jinsi shughuli za kuokoa zitakavyotekelezwa endapo vyombo vyao vitapata ajali baharini.

Bw Mwango aliwataja waliopokezwa vyeti kuwa manahodha waliohitimu vilivyo katika masomo yao ya ubaharia, hivyo akaeleza matumaini kuwa utiifu wa sheria za usafiri wa baharini Lamu utaimarika zaidi kinyume na ilivyokuwa awali.

“Kwa sababu manahodha waliopokezwa vyeti vya ubaharia Lamu wamehitimu ipasavyo,sitarajii sheria zinazoambatana na usafiri wa baharini kukiuka kiholela.Hii inamaanisha hata ajali ambazo tumekuwa tukishuhudia kila mara hapa Lamu na nchini zitapungua kutokana na mpango huu,” akasema Bw Mwango.

Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Lamu Magharibi, Michael Yator, pia alisisitiza haja ya mabaharia wa Lamu kutii sheria zote na kuepuka kubeba abiria wengi kupita kiasi ili kupunguza ajali.

Alisema idara ya usalama eneo hilo iko macho ili kuona kwamba sheria za usafiri wa baharini zinaheshimiwa vilivyo.

Naye Naibu Gavana wa Lamu, Abdulhakim Aboud aliahidi ushirikiano wa dhati kati ya serikali ya kaunti hiyo, KMA na wadau wengine katika kuimarisha usalama wa safari za majini Lamu.

“Ninawapongeza sana KMA kwa juhudi zao za kutoa mafunzo kwa manahodha wet una kuwapokeza vyeti wale waliofuzu. Tuendelee na ushirikiano huo huo,” akasema Bw Aboud.

Lamu iko na zaidi ya manahodha 5000 wanaotekeleza shughuli zao za usafiri wa baharini kwenye visiwa mbalimbali vya kaunti hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Nyuki wazua kizaazaa katika kituo cha mabasi cha Machakos

Wakurugenzi wa kampuni ya kuuza sukari wako na kesi ya...

F M