Dondoo

Mganga aonya pasta kwa kumchomea biashara

July 15th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

HAMISI, VIHIGA

KIOJA kilizuka eneo hili baada ya mganga kumshambulia pasta akimlaumu kwa kumharibia jina.

Kulingana na mdokezi, mganga alienda moja kwa moja hadi kwa boma la pasta na kuanza kumfokea huku akitishia kumwadhibu vikali.

Duru zinaarifu kwamba pasta alikuwa akiwakashifu wale waliopenda kutafuta huduma za mganga huyo.

Katika mahubiri yake, pasta alikuwa akimkemea mganga huyo huku akimuita ibilisi mkubwa anayewapora watu.

Habari zilipomfikia mganga alikasirika. “Una ujinga sana. Mbona usishughulike na mambo yako nami nishughulike na yangu,” mganga alimshtumu pasta.

Inasemekana pasta alimkemea mganga huyo huku akimtaka aondoke kwake mara moja. “Acha kuleta mashetani wako hapa. Ondoka haraka,” pasta alimkemea mganga.

Inadaiwa mganga alimuonya pasta kuacha kutaja jina lake kabisa. “Kila mtu afanye kazi yake. Kama unaona yako haikupi riziki basi njoo nikufunze yangu badala ya kuniharibia jina,” mganga alimshauri pasta.

Penyenye zinasema pasta alitishia kuwaita waumini wa kanisa lake kumtimua mganga.

“Ukitaka kuwaita waite. Usipokomesha uchochezi, walahi hutaamini kitakachokufanyikia na utakuja kwangu kunitafuta,” mganga alimtishia pasta.

Majirani wa pasta walibaki vinywa wazi. “Mwambieni huyu mtu wenu aachane na jina langu. Kanisani mwake hawezi kutamatisha mahubiri yake kama hajalitaja jina langu kwa ubaya. Nashuku ni pasta bandia,” mganga aliwaeleza majirani.

Inasemekana pasta aliudhika sana na semi za mganga. “Shetani ashindwe. Unadai kuwaponya watu lakini ni uongo mtupu. Umewahadaa watu wengi humu kijijini,”pasta alimfokea mganga.

Aliendeleza, “Siku ya nyani kufa inakaribia, nakwambia inakaribia kwa jina la Yesu, ondoka hapa.”