Habari Mseto

Serikali yawatuma Israel wanafunzi 96 kufundishwa ukulima wa kisasa

August 1st, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

KATIKA juhudi zake za kutatua shida ya uhaba wa chakula nchini, serikali imewatuma wanafunzi 96 nchini Israel kupokea mafunzo kuhusu ukulima wa kisasa.

Mpango huo umezinduliwa na Waziri wa Maji na Unyunyiziaji Simon Chelgui katika afisi yake iliyoko Maji House.

Kikundi hicho cha wanafunzi ambacho ni cha pili kinatarajiwa kupokea mafunzo kwa muda wa miezi 11.

“Kuwepo kwa chakula cha kutosha ni mojawapo ya nguzo za Ajenda Nne Kuu za serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na maji ni muhimu sana katika kufikia lengo hilo,” amesema Bw Chelgui.

Waziri Chelgui amedokeza kwamba serikali iko katika mikakati ya kuhakikisha kwamba ukulima wa unyunyiziaji mimea maji umefaulu nchini.

“Mafunzo hayo yatahusisha elimu ya kuchakata maji, ukulima wa unyunyiziaji na teknolojia katika ukulima,” amesema waziri.

Mafunzo

Wanafunzi hao watapokea mafunzo katika chuo cha Arava International Center for Agriculture Training (AICAT).

Ameongeza kwamba wizara yake itahakikisha kwamba miradi yote ya maji nchini imekamilika kwa wakati unaofaa ili kuboresha uzalishaji wa chakula.

Vilevile amedokeza kwamba ujenzi wa mabwawa kama vile Thwake, Siyoi Muruny, Yamo, Wamba na Karumenu tayari umeanza.