Habari Mseto

Taabani kwa kuongoza njama za kumuua mumewe na kudai fidia

August 14th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE aliyetalikiana na mumewe alifikishwa kortini Jumanne kwa madai alipanga njama za kumuua kisha adai alipwe fidia na kampuni ya bima.

Hakimu mwandamizi Mahakama ya Milimani Martha Mutuku alifahamishwa na wakili aliyemwakilisha Emmah Wangari Wangui kwamba Evans Karanja Mwangi, amejaribu juu chini kipenzi chake kishtakiwe pasi mafanikio.

“Bw Mwangi ambaye yuko hapa kortini amefanya kila awezalo Emmah Wangari Wangui ashtakiwe pasi ufanisi,” alisema wakili huyo.

Mahakama ilifahamishwa Bw Mwangi amesaka usaidi wa maafisa wa polisi kutoka kaunti ya Murang’a na Kiambu wamshike Wangari bila mafanikio.

“Wangui alikuwa akiishi na Mwangi lakini wametengana. Mwangi amekuwa akisaka polisi wamtie nguvuni wamshtaki,” wakili anayemwakilisha alidokeza.

Lakini mahakama ikaelezwa mshtakiwa amepata afueni baada ya mahakama kuu kutoa agizo kumzuia mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP kumfungulia mashtaka Wangari.

Bi Mutuku alikabidhiwa nakala za maagizo ya Jaji Jessie Lesiit wa Mahakama kuu Nairobi na Jaji Christine Meoli wa Mahakama kuu ya Kiambu.

“Ili hii mahakama isionekane ikaidi agizo la mahakama kuu , Wangari hatasomewa mashtaka lakini mshtakiwa mwenza Peter Mwaniki Wanjiku atajibu mashataka saba,” Bi Mutuku aliagiza.

Pia alimwamuru kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda, awasiliane na mahakama kuu kubaini ikiwa maagizo hayo yamo jinsi alivyoelezwa na wakili wa Wangari.

Bi Mutuku alimwamuru Wangari afike tena kortini Agosti 27, 2019 , Bw Gikunda abaini ikiwa maagizo hayo ni ya kweli.

Aliposomewa mashtaka Mwaniki alikanusha alighushi kitambulisho cha kitaifa cha Mwangi alichowakabidhi maafisa wa makampuni matatuya bima ya ICEA Lion Life, APA na Britam kusajiliwa dhidi ya bima za ajali.

Pia alishtakiwa kujifanya Bw Mwangi kwa maafisa wa makampuni hayo matatu ya bima Juni 2018.

Hakimu aliwaachilia Wangari na Mwaniki kwa dhamana ya Sh500,000.