Michezo

Kinyago United wazidi kutesa KYSD

September 11th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

CHIPUKIZI wa Kinyago United waliendelea kuimarisha kampeni zake kutetea ubingwa wa Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 walipobana Tico Raiders mabao 3-1 ugani KYSD Kamukunji, Nairobi.

Nao vijana wa State Rangers waliona giza walipokubali kunyukwa magoli 5-2 na Volcano FC huku Sharp Boys ikiyeyusha alama mbili muhimu baada ya kulazimishwa sare tasa na Young Achievers.

Wachezaji wa Kinyago wa kocha, Anthony Maina waliingia mjengoni tayari kuonyesha ubabe wao huku wakilenga kutia kapuni ushindi wa pointi zote tatu.

Wapigagozi hao walionyesha mchezo safi na kuzima ndoto ya wapinzani wao kupitia Austine Okoth, Abedbego Wawire, Jahson Wakachala waliofuma bao moja kila mmoja. Naye Gevean Owino aliitingia Tico Raiders bao la kufuta machozi.

”Tumeapa kuwa raundi kamwe hatutaki kuteleza mbali tumepania kuendeleza mtindo wa kutembeza vipigo dhidi ya wapinzani wetu,” nahodha wa Kinyago Samuel Ndonye alisema na kuongeza kuwa katika mpango mzima wamepania kushiriki kila mechi kama fainali ili kuendelea kujiweka pazuri kuhifadhi taji hilo msimu huu.

Wachezaji wa Sharp Boys FC wanaoshiriki kipute cha KYSD. Picha/ John Kimwere

Kinyago inazidi kufana baada ya kushinda mechi zote tisa ambazo imeshiriki kwenye juhudi za kutafuta ubingwa wa taji hilo kwa mara ya 13. Wafungaji wa Volcano FC walikuwa Mohammed Ali alipopiga mbili safi, nao Abdirazak Abdullahi, Shakri Abdifatah na Mohammed Ahmed kila mmoja alicheka na wavu mara moja. Naye Felix Ouma aliifungia State Rangers mabao yote mawili.

Kwenye matokeo hayo, Young Elephant ilirandwa mabao 2-1 na Pumwani Foundation, Fearless FC iliichapa Lehmans goli 1-0, MASA ilikung’utwa magoli 4-1 na Locomotive FC, Gravo Legends ilidunga Fearless FC magoli 5-0 huku Pro Soccer Academy ikitwaa mabao 5-2 dhidi ya Pumwani Ajax. Ngarambe hiyo inayojumuisha timu 16 inapigiwa upatu kuzua upinzani wa mkali kuliko misimu iliyopita.