Michezo

Nyayo tayari kuandaa KPL

September 13th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

BAADA ya kufungwa kwa miaka miwili kutokana na shughuli za ukarabati, uwanja wa kitaifa wa Nyayo sasa utaanza kutumika kuanzia mwishoni mwa wiki.

AFC Leopards ambayo imekuwa ikiutumia uwanja huo kwa mechi zake za nyumbani, itaikaribisha Kariobangi Sharks hapo Jumapili katika pambano la Ligi Kuu ya Kenya (KPL), kuanzia saa tisa.

Mechi ya mwisho kuchezewa uwanjani humo ilikuwa ya Mashemeji Derby kati ya AFC Leopards na Gor Mahia mnamo Agosti 27, 2018 ambayo ilimalizika kwa sare ya 1-1.

Kadhalika, uwanja huo ulitumiwa kuandaa sherehe za Siku Kuu ya Jamhuri Dei za 2018, lakini sasa utafunguliwa rasmi kuandaa mashindano mbali mbali pamoja na ratiba za kimataifa.

Katubu Mkuu wa Leopards, Oliver Sikuku alithibitisha kwamba mechi yao ya wikendi itachezewa katika uwanja huo.

“Tumekubaliwa kuanza kurejea Nyayo Stadium baada ya shughuli za ukarabati kukaribia kumalizika. Ukarabati unakaribia kukamilika, lakini sehemu kubwa iko tayari kuanza kuandaa mechi yoyote.

“Wasimamizi wa uwanja wametukubalia kuanza kuutumia, lakini tumeambiwa tuwaonye mashabiki wazingatie nidhamu ya hali ya juu.”

Nyayo Stadium huvutia mashabiki wengi wa Gor Mahia na AFC Leopards kwa kuwa unapatikana karibu na jiji kuu la Nairobi badala ya Machakos ambao mashabiki hulazimika kutumia pesa nyingi za kugharimia nauli.

Matumaini kwa AFC Leopards

Leopards imewekewa matumaini makubwa ya kuandikisha matokeo bora dhidi ya Kariobangi Sharks baada ya kufanya usajili wa nguvu majuzi.

Mabingwa hao wa KPL mara 13 wamesajili wanasoka kadhaa hodari, akiwemo mshambuliaji matata Mark Makwatta.

Mbali na mshambuliaji huyo wa kimataifa, kadhalika, Ingwe ilifanikiwa kuwapata Kevin Kimani kutoka Mathare United, Clyde Senaji kutoka Tusker FC pamoja na beki wa upande wa kushoto Washington Munene kutoka Wazito FC.

Wengine waliojiunga na Ingwe ni beki Robert Ayala Mudenyi kutoka Sony Sugar, Soter Kayumba na Collins Shivachi.

Leopards pia imeisuka upya safu yake ya ushambuliaji kwa kuwasajili Paul Were, Ismail Diarra raia wa Mali ambaye aliwahi kuchezea klabu za Azam, Al Ismaily na DC Motema Pembe ya DR Congo pamoja na Vincent Abamahoro kutoka Kiyyovu Sports ya Rwanda.

Kadhalika Ingwe ilifanikiwa kumtwaa kiungo wa kimataifa, Tresor Ndikumana ambaye atasaidiana na Whyvonne Isuza huku lango likilindwa vikali na Benjamin Ochan ambaye alijaza nafasi ya Eric Ndayishimiye.