Habari

Hakuna haja ya mageuzi ya Katiba, wasema Ghai na Mohamed

September 24th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WANASHERIA wawili waliohusika katika utayarishaji wa Katiba ya sasa wamepuuzilia mbali shinikizo mbalimbali za mageuzi ya Katiba wakisema hatua hiyo si suluhu kwa matatizo yanayolikumba taifa hili.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Profesa Yash Pal Ghai na aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge kuhusu Marekebisho ya Katiba, Abdikadir Mohamed wamesema Jumanne kile kinafaa kupewa kipaumbele ni utekelekezaji kwa ukamilifu wa yaliyomo katika hati hiyo.

“Matatizo kama vile uongozi mbaya, ufisadi na kutojumuishwa kwa makabila yote katika serikali – ambayo yamekuwa yakushughulikiwa na Jopokazi la Maridhiano (BBI) – yanaweza kushughulikiwa ipasavyo ikiwa sura ya sita itatekelezwa kikamilifu. Na hatuhitaji mageuzi ya ‘Punguza Mizigo’ ikiwa hitaji la uadilifu wa viongozi litapewa uzito,” Profesa Ghai akawaambia wabunge.

Amesema utekelezaji wa vipengee mbalimbali vya Katiba ya sasa kwa ukamilifu utakuwa wa manufaa makubwa na gharama ya chini kwa mlipa ushuru kuliko mageuzi ya Katiba kupitia kura ya maamuzi.

“Tunawaambia kuwa kura ya maamuzi itagharimu mlipa ushuru takriban Sh15 bilioni. Hizi ni pesa ambazo bila shaka zitaokolewa ikiwa Katiba ya sasa itatekelezwa kikamilifu,” Profesa Ghai akaiambia Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji wa Katiba (CIOC).

Maendeleo

Kwa upande wake Bw Mohamed amesema kando na sura ya sita ya Katiba, ipo haja kwa wabunge na wadau wengine kushinikiza utekelezaji ugatuzi ili kufanikisha azma ya usambazaji wa maendeleo kwa usawa katika maeneo yote ya nchi.

“Kwa mfano, matatizo yanayokumba sekta ya afya yanaweza kushughulikiwa ipasavyo ikiwa rasilimali zote zitaelekezwa katika serikali za kaunti. Kimsingi hatuhitaji wizara ya afya katika ngazi ya Serikali ya Kitaifa kwa sababu majukumu yote ya afya yamegatuliwa,” akasema.

Kulingana na Bw Mohamed, ambaye aliwahi kuhudumu kama Mbunge wa Mandera ya Kati katika katika Bunge la 10, amesema mipango ya mageuzi ya Katiba kupitia mswada wa ‘Punguza Mizigo’ BBI au “Ugatuzi Initiative” inatumiwa na wanasiasa kuendeleza ajenda zao katika uchaguzi mkuu wa 2022.