Habari Mseto

Sababu ya makahaba kuandamana mjini Thika

October 1st, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MAKAHABA mjini Thika waliandamana Ijumaa wiki jana wakitaka maslahi yao kuendeshwa na Shirika la National Organisation of Peer Educators (NOPE).

Makahaba hao kutoka Ruiru, Githunguri, Kiambu na Thika walisisitiza kwamba watazidi kuteta hadi matakwa yao yaweze kuchunguzwa ipasavyo.

Walisema Kaunti ya Kiambu imesitisha shughuli za shirika la NOPE na kuwajumuisha makahaba hao katika shirika la Liverpool VCT ambalo litaendelea kuwashughulikia.

Hata hivyo, walisema shirika la NOPE chini ya meneja wake Barrack Ondieki limekuwa likiwapokea kwa ukarimu na kuwapatia ushauri mzuri wa kimatibabu.

Wengi wao ambao hawakutaka kutajwa majina hadharani, walisema wamejishughulisha na biashara hiyo kwa miaka kumi kuendelea ambapo hata wanalea familia zao kupitia kazi hiyo.

Walisema wamekuwa na maadui wengi ambao huwahangaisha kila mara usiku wakijaribu kujitafutia riziki.

Makahaba hao ni wenye umri wa kati ya miaka 30 na 52 na ambao wamejitolea kuendesha biashara hiyo ili kujikimu kimaisha.

Wengine wanaoingilia kazi yao ni wafanyabiashara ambao hawataki kuwaona katika sehemu zao za kazi, walisema.

Matibabu

Walisema shirika hilo la NOPE limekuwa mstari wa mbele kuwapatia matibabu wakati wote wanapougua kwa njia moja ama nyingine.

Hata walisema ya kwamba wakati mwingi walipokuwa katika mkono wa sheria, meneja wao alikuwa wa kwanza kuwatoa gerezani.

Sasa wanahofia maslahi yao hayatatiliwa maanani na hakuna mwingine atakuwa na utu kama meneja huyo ambaye alijitolea kwa kila njia.

Wakijitetea nje ya afisi yao mjini Thika, makahaba hao walisema wanahofia biashara yao itadorora kwa sababu maadui wao watafanya juhudi kuona ya kwamba hawafanyi biashara hiyo kwa amani.

Mashirika hayo yote mawili yanaendesha shughuli zake chini ya mwavuli wa USAID.

Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi umebainisha kuwa Kaunti ya Kiambu pekee ina makahaba wapatao 10,000.

Nao mji wa Thika pekee una idadi ya makahaba wapatao 5,800.

Makahaba hao walionekana kutetea hali yao kwa nguvu huku wakisema chakula chao cha kila siku kiko katika Jumba la NOPE.