Habari

Vijana walia wazee wakicheka

October 16th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU na NICHOLAS KOMU

WAKONGWE waliohudumu serikalini awali wanaendelea kuitwa kutoka kustaafu na kuteuliwa kwenye nyadhifa kuu na serikali ya Jubilee, huku maelfu ya vijana wakiendelea kulia kwa ukosefu wa ajira.

Hii ni licha ya ahadi ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto kwenye kampeni zao 2017 kwamba wangeweka mikakati ya kubuni ajira kwa vijana.

Tangu alipoanza kuhudumu kwa kipindi cha pili, Rais Kenyatta ameendelea kuwateua wazee, hali inayoibua maswali ya ikiwa serikali amefumbia macho janga la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

Uteuzi wa juzi, ambao umeibua shutuma kali ni wa Bi Mary Wambui, ambaye alihudumu akiwa mbunge wa eneo la Othaya kati ya 2013 na 2017. Bi Wambui ameteuliwa mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Kuhusu Ajira (NEA).

Wakenya wengi waliokosoa uteuzi huo wametilia shaka uwezo wa Bi Wambui, wakieleza tashwishi kuhusu vigezo vilivyozingatiwa kumpa cheo hicho. Wakenya kwenye mitandao walisema mbunge huyo wa zamani hataongeza manufaa yoyote katika NEA.

Seneta Maalum Millicent Omanga na aliyekuwa mwaniaji urais, Bw Mohamed Abduba Dida, walisema uteuzi huo unaonyesha kuwa serikali haijajitolea kukabili changamoto zinazowakabili vijana.

Hata hivyo, Bi Wambui alijitetea vikali Jumanne, akisema kuwa ana uwezo wa kutekeleza kazi hiyo.

“Nilipata uteuzi huo kwa sababu ninafaa kuliko wanaolalamika. Nina tajriba ya kutosha kutekeleza majukumu nitakayohitajika kufanya,” akasema Bi Wambui kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Baadhi ya wazee waliostaafu lakini wakaitwa mapumzikoni kuhudumu serikalini ni aliyekuwa Seneta wa Kitui Bw David Musila, 76 ambaye ni mwenyekiti wa Makavazi ya Kitaifa Kenya (NMK), Makamu wa Rais wa zamani Bw Moody Awori, 92 kuwa mwanachama wa Hazina ya Michezo, Sanaa na Ustawishaji Jamii na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Julius Karangi, 68 anayehudumu akiwa mwenyekiti wa Hazina ya Kitaifa ya Uzeeni (NSSF).

Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Bw Francis Muthaura, 72 ambaye ni mwenyekiti wa Mradi wa Kustawisha Bandari ya Lamu (LAPSSET) na pia ndiye mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushuru (KRA), na mfanyabiashara Manu Chandaria, 89 ambaye ni Chansela wa Chuo Kikuu cha Kiufundi Kenya (TUC).

Pia kuna Bi Beth Mugo, 80, ambaye ni Seneta Maalum wa Chama cha Jubilee; Bw Marsden Madoka, 75, mwanachama wa Hazina ya Kitaifa ya Kuwasimamia Watu Walemavu (NFD); Bw Chris Obure, 75 aliyeteuliwa Naibu Waziri katika Wizara ya Uchukuzi na Miundomsingi, Bw Jeremiah Matagaro (mwenye umri wa zaidi ya miaka 60) kama mwenyekiti wa Kamati ya Kutoa Ushauri kwa Mashirika ya Serikali (State Corporations Advisory Committee-SCAC) na Bi Esther Murugi, 69, kama mwanachama wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kati ya wengine.

Licha ya mwelekeo huo wa kupendelea wakongwe, Rais Uhuru Kenyatta amejitetea vikali, akisema kuwa anawaamini zaidi wazee kuliko vijana.

“Ukiona jinsi vijana tuliowaamini kusimamia nyadhifa za umma wanavyoshiriki ufisadi, ni afadhali kumteua mzee kama Awori, ambaye ninaamini atalinda fedha za umma ili kuhakikisha Wakenya wanafaidika kutokana na fedha zao,” akasema Rais Kenyatta alipojitetea kuhusu hatua ya kumteua Bw Awori.