Habari

Presha yabana Uhuru

October 18th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta anakabiliwa na presha kali kutimiza ahadi zake kwa Wakenya huku kipindi chake cha pili uongozini kikielekea ukingoni.

Mnamo Jumatano Rais Kenyatta alikiri kuwa amechoka.

Wadadisi wanasena ni kutokana na presha hii ndiposa yumo mbioni kuzindua kila aina ya miradi hata kabla ya mingine kukamilika ili kuonyesha Wakenya kuwa serikali yake inatekeleza ahadi ilizowapa.

Hii inatokana na Rais kutambua kuwa ni miaka miwili na nusu pekee iliyobaki kipindi chake cha pili kimalizike kukiwa na hatari ya ahadi zake kukosa kutimia.

Serikali yake imekopa matrilioni ya pesa na kuna presha ya kulipa madeni hayo. Kufikia Juni mwaka huu deni la Kenya lilikuwa zaidi ya Sh5.8 trilioni na mwezi huu mashirika wafadhili yalionya kuwa limevuka mipaka.

Dalili zinaonyesha wazi hali ya uchumi ni mbaya kutokana na kampuni nyingi kufungwa na kuwafuta wengi, bei ya bidhaa kupanda, sekta ya kilimo inaporomoka, uhalifu umeongezeka, mamilioni ya vijana hawana kazi, chama chake cha Jubilee kimesambaratika na Ajenda Nne Kuu zimo kwenye hatari ya kufeli.

Changamoto hizi zimemfanya kuzindua na kutetea miradi ambayo wadadisi wanatilia shaka umuhimu wake kwa Wakenya sasa na miaka ijayo.

Mnamo Jumatano alitetea ujenzi wa awamu ya pili ya reli ya SGR kutoka Nairobi hadi Suswa, Kaunti ya Narok ambayo wadadisi wanasema ilikuwa sawa na kuzindua reli isiyoelekea popote.

Kulingana na wanauchumi, Rais angesubiri angalau SGR ifike Naivasha kwanza badala ya kuizindua.

“Hatua ya rais inaonyesha mtu aliye na presha nyingi ya kutimiza ahadi zake kwa Wakenya. Inabidi achukue kila fursa kuonyesha kwamba serikali yake inafanya kazi. Muda uliobaki ni mchache sana kuweza kutekeleza ajenda zake na kuacha kumbukumbu,” alikiri mbunge mmoja wa chama cha Jubilee.

Hata hivyo, Rais alitetea reli hiyo na kuwataja wanaoikosoa kuwa waliokosa kuwa na wajinga.

Siku moja kabla ya kuzindua reli hiyo, Rais Kenyatta alizuru mjini Kisumu kwa mara ya saba kukagua ukarabati wa bandari unaoendelea.

Bandari hiyo ilitarajiwa kuzinduliwa Agosti katika hafla iliyopangiwa kuhudhuriwa na marais sita wa nchi za kanda lakini ikaahirishwa dakika za mwisho ilipobainika serikali ingepata aibu kwa sababu haikuwa tayari.

Duru zinasema Rais anataka kuzindua bandari hiyo ili kushawishi marais wa Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na Sudan Kusini kukumbatia SGR.

Baada ya SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi kukamilika, Rais amejipata mwenye presha kubwa baada ya wakazi wa Pwani kupinga maamuzi ambayo yanavuruga hali ya biashara zao.

Maamuzi hayo ni pamoja na agizo kuwa lazima mizigo yote isafirishwe kwa SGR na pia kukabidhi usimamizi wa eneo la mizigo la Kipevu kwa kampuni ya kibinafsi. Mahakama imesimamisha ubinafsishaji huo.

Wadadisi wanasema kasi ya serikali kuzindua miradi ili kuonekana inafanya kazi inaifanya kukiuka sheria, jambo ambalo linageuka kuwa aibu mahakama inapoingilia.

Rais pia anajikuna kichwa kwa kuhangaishwa na vijana ambao wakati wa kampeni aliwaahidi atabuni nafasi za kazi kwao. Lakini hilo limekuwa ndoto na vijana wanaendelea kulalamika kuwa aliwadanganya na hawajali.

Rais Kenyatta alinuia kutimiza ahadi hii kupitia ajenda zake nne kuu za kutoa makazi nafuu, utoshelezaji wa chakula, afya kwa wote na viwanda.

Akiwa Suswa alipozindua kituo cha reli ya kisasa, Rais Kenyatta aliwaambia Wakenya kuwa SGR itasaidia wawekezaji kuanzisha viwanda eneo hilo ili vijana wapate kazi.

Ujenzi wa barabara

Alitoa matamshi kama hayo alipozindua ujenzi wa barabara ya moja kwa moja kutoka JKIA hadi Westlands ambapo alisema aliagiza mwanakandarasi kuajiri vijana kutoka mitaa ya jiji la Nairobi na viunga vyake.

Kufikia sasa utekelezaji wa ajenda zake umekumbwa na vizingiti ikiwa ni pamoja na ukosefu wa fedha, jambo lililompa presha hadi wizara, idara na mashirika ya serikali yakalazimika kukata bajeti ili kutenga pesa za kufanikisha ajenda hizo.

Kwenye ilani kwa wizara na mashirika ya serikali, Kaimu Waziri wa Fedha Ukur Yattani alisema hatua hii inalenga kukusanya Sh131 bilioni kufadhili ajenda nne kuu za serikali.

Presha ya kuacha kumbukumbu nayo ilimfanya Rais kushinikiza kubadilishwa kwa mtaala wa elimu licha ya upinzani kutoka kwa wadau.

Mtaala mpya wa CBC ulianza kutekelezwa mwaka huu hata kabla ya kupigwa msasa.

Kulingana na wadadisi, Rais Kenyatta anakabiliwa na wakati mgumu kutimiza ajenda zake katika mazingira magumu ya kiuchumi na kisiasa.

Changamoto nyingine ni kufifia kwa moto wa kukabiliana na ufisadi.