Michezo

Upo uwezekano wa Manchester United kuagana na Paul Pogba

October 19th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TETESI mpya zimeibuka kuhusu uwezekano wa Manchester United kuagana na Paul Pogba baada ya kiungo huyo kukutana na kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane.

Wafaransa hawa, ambao wote ni washindi wa Kombe la Dunia, walizungumza kando ya bwawa la kuogelea mjini Dubai baada ya kukutana wakati ligi ilipisha awamu ya mechi za timu za taifa.

Nyota wa United, Pogba, ambaye anatarajiwa kukosa mechi ya Ligi Kuu dhidi ya viongozi Liverpool akiuguza jeraha la kifundo, amekuwa akiendelea kupata nafuu katika nchi ya Milki za Kiarabu.

Zidane alitaka kusaini Pogba aliyegharimu United Sh11.9 bilioni kutoka Juventus, lakini Waingereza hao walikataa mavizio hayo, wakisisitiza mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 26 hayuko sokoni.

Hata hivyo, wakala wa Pogba, Mino Raiola, ambaye huwa mtu wa kutoa dukuduku waziwazi, alitangaza kuwa Pogba anatamani kuhama uwanjani Old Trafford.

Mchezaji huyo mwenyewe alikiri kuwa pengine muda wake wa kutafuta “changamoto mpya” ulikuwa umewadia. United haikulegeza kamba. Pogba anasalia na miaka miwili katika kandarasi yake na United pamoja na uwezekano wa kuongezwa mwaka mmoja.