4 waaga ajali zikiendelea kuongezeka

4 waaga ajali zikiendelea kuongezeka

LUCY MKANYIKA na WINNIE ATIENO

WATU wanne walifariki jana na wengine 20 wakajeruhiwa katika ajali tofauti zilizotokea eneo la Voi kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.

Katika ajali ya kwanza iliyosababisha vifo eneo la Manyani, basi la kampuni ya Dreamline liligongana na lori. Waliopoteza maisha yao ni madereva wa magari hayo mawili, tani boi wa lori na abiria wa kike.Kamanda wa polisi wa Voi, Bw Bernastein Shari, alisema abiria 17 walijeruhiwa wakakimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Moi.

Alisema dereva wa basi hilo lililokuwa likielekea Mombasa kutoka Busia, alijaribu kupita lori lingine ndipo akagongana na lori lililokuwa likielekea upande wa pili.“Watu wanne walikufa papo hapo. Ilituchukua saa kadhaa kuondoa miili ya dereva wa lori na tani boi kwa vile walikuwa wamekwama,” akasema.

Katika kisa cha pili, madereva wa lori na matatu zilizogongana walipata majeraha mabaya katika eneo la Maungu.Bw Shari alisema lori liligonga matatu upande wa nyuma wakati dereva wa matatu alikuwa amepunguza kasi ili apite matuta barabarani mjini Maungu.

Wawili hao walitibiwa katika hospitali ya River Jordan, kisha baadaye wakahamishwa hadi Hospitali ya Moi kwa matibabu zaidi.“Nawaomba madereva wawe waangalifu barabarani. Ajali hizi zinaongezeka na kutishia maisha ya wasafiri,” akasema.

Msimamizi mkuu wa Hospitali ya Moi, Dkt Felix Kimotho, alisema wiki hii hospitali hiyo imepokea majeruhi kutoka kwa ajali tatu tofauti na baadhi yao wakahamishwa hadi Kaunti ya Mombasa kupokea matibabu maalumu. Kwingineko, mamia ya abiria walitatizika kwa muda katika eneo la Kibarani, barabara ya Mombasa-Nairobi, baada ya kasha la kubeba mizigo kuanguka kutoka kwa lori na kusababisha msongamano mkubwa barabarani.

Baadhi ya abiria waliokuwa wakielekea Mombasa kutoka bara walilazimika kushuka na kutembea huku watalii wa kigeni waliokuwa wakielekea mjini kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi, pia wakilazimika kuabiri bodaboda.

You can share this post!

Hakuna sherehe za pombe haramu

TAHARIRI: Serikali iweke sera za kudhibiti kupandisha nauli

T L