Michezo

Kabras Sugar yalipua Western Bulls 47-0 mjini Kakamega

December 7th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa mwaka 2016 Kabras Sugar wameendelea kutoa dozi kali kwa wapinzani kwenye Ligi Kuu ya raga ya wachezaji 15 kila upande (Kenya Cup) baada ya kulipua majirani Western Bulls 47-0 mjini Kakamega, Jumamosi.

Wanasukari wa Kabras sasa wameshinda mechi saba mfululizo kwenye ligi hii ya klabu 12.

Kabras itazuru jijini Nairobi kwa mechi yake ijayo kumenyana na Homeboyz, ambayo pia imetuma onyo kwa wanasukari hao kwa kupepeta Kisumu 53-3 mjini Kisumu.

Nao mabingwa watetezi KCB, ambao walikubali kichapo cha alama 19-6 katika mechi yao iliyopita dhidi ya Kabras, waliandikisha ushindi wao wa sita katika mechi saba walipolaza wenyeji wao Mwamba 29-15 uwanjani Nairobi Railway jijini Nairobi.

Washikilizi wa rekodi ya mataji mengi ya Kenya Cup, Nondies (17) ndio wameandikisha matokeo ya kushangaza katika raundi hii ya saba baada ya kunyamazisha washindi wa mwaka 2013 na 2014 Nakuru 31-22 uwanjani Jamhuri Park. Nondies walikuwa wameteleza katika mechi kadhaa na hata kuingia katika mduara hatari wa kutemwa nao Nakuru walikuwa wameamka baada ya kuanza msimu vibaya.

Matokeo ya raundi ya saba (Desemba 7, 2019):

Kabras Sugar 47-0 Western Bulls

Mwamba 15-29 KCB

Impala Saracens 26-19 Kenya Harlequin

Nondescripts 31-22 Nakuru

Blak Blad 15-25 Menengai Oilers

Kisumu 3-53 Homeboyz