Habari

Ruto atupia Kalonzo ndoano

December 28th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO na TITUS OMINDE

NAIBU wa Rais William Ruto anaonekana kumnyemelea kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka katika maandalizi ya kinyang’anyiro cha urais 2022.

Licha ya Bw Musyoka kusisitiza kuwa hakuna mazungumzo yanayoendelea baina yake na Dkt Ruto, wanasiasa wa kundi la Tangatanga, jana walithibitisha kuwa muungano baina ya wawili hao unanukia.

Wanasiasa wa Tangatanga wakiongozwa na mbunge wa Kimilili, Bw Didmas Barasa na mwenzake wa Soy, Bw Caleb Kositany walisema kuwa mazungumzo baina ya Naibu wa Rais Ruto na Bw Musyoka yamenoga na huenda wakabuni muungano wa kisiasa.

Dkt Ruto, kupitia kwa mtandao wa Twitter, Ijumaa alimkaribisha Bw Musyoka ndani ya Jubilee huku akisema kuwa chama hicho tawala ndicho kilicho na maono.

Naibu wa Rais alimkaribisha Bw Musyoka baada ya kiongozi huyo wa Wiper kusema kuwa atakuwa upande ambao Rais Uhuru Kenyatta atakuwa katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

“Karibu Stevo (Stephen Kalonzo) katika chama cha Jubilee chake (Uhuru) Kenyatta. Hiki ndicho chama kilicho na maono. Mambo tuliyoyapa kipaumbele ni utekelezaji wa Ajenda Nne za maendeleo na kubadilisha maisha ya Wakenya kwa mujibu wa manifesto ya Jubilee,” akasema Dkt Ruto huku akiwa ameambatanisha video ya Bw Musyoka akisema kuwa hatatenganishwa na Rais Kenyatta.

Mwaliko huo wa Dkt Ruto umefasiriwa kuwa ishara kwamba yuko tayari kushirikiana na Bw Musyoka kuhakikisha kuwa chama cha Jubilee kinasalia mamlakani baada ya uchaguzi wa 2022.

Rais Kenyatta ameonekana kujitenga na shughuli za Jubilee na tangu kuchaguliwa kwa muhula wa pili mnamo Oktoba 26, 2017, hajawahi kuandaa mkutano wa viongozi wa chama hicho.

Alipokuwa akihutubia viongozi wa Ukambani nyumbani kwake katika eneo la Yatta, mapema wiki hii, alisema kuwa ataunga mkono mwaniaji wa urais atakayeungwa mkono na Rais Kenyatta.

“Alipo ndugu yangu Uhuru Muigai Kenyatta katika uchaguzi wa 2022, nitakuwa hapo. Kuna baadhi ya watu wanaotaka Kalonzo kutoka huko nianguke,” akasema Bw Musyoka.

Wiki iliyopita, aliyekuwa Seneta wa Machakos, Bw Johnstone Muthama alidokeza kuwa atahakikisha kuwa Dkt Ruto na Bw Musyoka wanaunda muungano wa kisiasa kabla ya 2022.

Bw Musyoka, hata hivyo, alijitokeza na kupuuzilia mbali kauli hiyo ya Bw Muthama.

Jumatano, Bw Muthama alimshambulia kiongozi wa Wiper akidai kuwa amekuwa akitumia eneo la Ukambani kujipendekeza mbele ya Rais Kenyatta.

Wakizungumza mnamo Alhamisi katika Shule ya Msingi ya Natwana katika eneobunge la Soy, Bw Barasa na Bw Kositany walisema kuwa Bw Musyoka ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamekuwa wakifanya mazungumzo na Naibu wa Rais ili kubuni muungano utakaombwaga kiongozi wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi mkuu ujao.

“Bw Odinga anataka kutumia ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) kutatiza ndoto ya Dkt Ruto kuingia Ikulu. Naibu wa Rais anajua njama yao na ameendelea kuweka mikakati ya kuwakabili,” akasema Bw Baraza.

“Nataka kumwambia Tinga (Bw Odinga) kuwa hata sisi tuna ubongo na tumeanza mazungumzo na Bw Kalonzo Musyoka pamoja na viongozi wengine wapendao maendeleo tumenyane naye 2022,” akaongezea.

Kauli ya Bw Baraza iliungwa mkono na Bw Kositany aliyesema kuwa mlango wa kambi ya Dkt Ruto ‘uko wazi na viongozi wanaotaka kujiunga naye wanakaribishwa.’