Michezo

TWAJA: Mamchester United yaanza kubishia hodi nafasi ya nne

December 30th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

BURNLEY, Uingereza

MANCHESTER United imeanza kubishia hodi nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kukamilisha mwaka 2019 kwa kishindo Jumamosi.

Ilizamisha wenyeji Burnley 2-0 kupitia mabao ya Anthony Martial na Marcus Rashford uwanjani Turf Moor.

Vijana wa kocha Ole Gunnar Solskjaer walijinyanyua kwa haraka baada ya kuchapwa 2-0 na Watford katika mechi iliopita na sasa wataingia mwaka 2020 na matumaini mapya wanaweza kufuzu kushiriki Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.

“Tunataka kuingia mduara wa klabu nne za kwanza na hatuko mbali. Hiyo ndio changamoto yetu sasa. Tulikaribia sana kumaliza msimu uliopita kwa kishindo, lakini tukafifia. Sasa, vijana wangu walifuta kichapo dhidi ya Watford na nimewapatia changamoto watafute kuwa katika klabu nne-bora. Nimefurahishwa sana nao,” alisema raia huyo wa Norway.

“Nadhani tulikuwa wazuri sana katika kipindi cha kwanza. Tulidhibiti na kutawala kipindi hicho,” aliongeza Solskjaer.

“Tulishuhudia matukio kadhaa ndani ya kisanduku chetu katika kipindi cha pili kwa sababu Burnley walikuwa wakishambulia vilivyo, lakini ngome yetu ilisimama imara.”

Ili kutimiza ndoto ya kumaliza ndani ya mduara wa nne-bora, Martial na Rashford wataendelea kutegemewa na walidhihirisha umuhimu huo wao walipofungia United mabao katika mechi iliokuwa na nafasi chache sana nzuri za kufunga.

Mojawapo ya vitu vizuri Solskjaer alishuhudia katika mechi hiyo ni kuwa kwa mara ya kwanza United haikufungwa bao baada ya kushindwa kufanya hivyo katika mechi 14 zilizopita.

“Sisi ni timu ambayo hatujakuwa tukipatiana nafasi nyingi, ingawa ikabu na mambo mengine ya kimsingi yamekuwa yakitusumbua,” alisema beki ghali duniani Harry Maguire, ambaye United ilitumia Sh10.5 bilioni kumnunua kutoka Leicester mwezi Agosti kujaribu kupunguza makosa katika safu ya ulinzi.

Burnley haijapata ushindi dhidi ya United tangu mwaka 2009 na haikuonekana kama inaweza kubadilisha mkondo huo.

Rashford alikuwa wa kwanza kupatia wasiwasi lango la Burnley alipopiga shuti lake nje ya mlingoti baada tu ya dakika 20 za kwanza.

Pasi safi

Hata hivyo, Burnley ya kocha Sean Dyche ilijichimbia kaburi kabla ya mapumziko pale Charlie Taylor alipoteza mpira uliochukuliwa na Andreas Perreira ambaye alimegea Martial pasi safi iliokamilishwa kwa ustadi na Mfaransa huyo.

Phil Bardsley kisha alisukuma kiki nzito lililomlazimu kipa David De Gea kufanya kazi ya ziada kuondosha. United hatimaye ilipata kuzamisha kabisa matumaini ya Burnley katika dakika za lala salama.

Daniel James aliongoza mashambulizi baada ya Burnley kuzimwa ikitafuta bao la kusawazisha na Rashford akapata bao lake la 16 msimu huu.