Habari Mseto

Nzige sasa waharibu mimea Baringo na Turkana

January 21st, 2020 2 min read

NA BARNABAS BII, SAMMY LUTTA na FLORAH KOECH

NZIGE waliovamia sehemu mbalimbali za nchi sasa wametua katika Kaunti za Turkana na Baringo.

Wameharibu hekta kadhaa za mimea na kusababisha hofu ya upungufu wa chakula katika maeneo hayo ambayo hukumbwa na ukame kila mara.

Wadudu hao waharibifu wameingia katika Kaunti Ndogo ya Loima, vijijini Lolemgete, Kankurumeri, Kanyangapus, Kankuridio na Moru Edou.

Kwa mujibu wa Naibu Chifu wa Kapual, Bw David Eteleg, nzige hao walionekana wakila mimea ambayo hutegemewa kwa lishe ya mifugo.

“Wameturudisha nyuma katika mafanikio tuliyopata kwa uzalishaji chakula cha kutosheleza mahitaji ya wakazi licha ya kuwa serikali ya kaunti ilifanikiwa kuwazuia kuenea miaka iliyopita,” akasema Bw Eteleg.

Wakazi walisema mwaka uliopita, mimea katika ardhi ya ukubwa wa ekari zaidi ya 10,000 iliharibiwa na nzige.

Ripoti kutoka kwa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) ilisema kuwa, wadudu hao wataingia Uganda watakapoondoka Baringo na Turkana.

“Tunataka serikali na washirika wetu wa kimaendeleo wachukue hatua haraka kuangamiza wadudu hawa kwa kunyunyiza dawa kutoka angani,” akasema Bw Eteleg.

Wakazi wa kata ndogo ya Kapua walionekana wakitumia mbinu za kienyeji kama vile kupuliza firimbi kuwashtua wadudu hao ili watoke katika mashamba yao.

Bw Jacob Ekwam ambaye ni mfugaji alisema kando na kuharibu mimea, nzige wanachafua maji yanayotegemewa na wenyeji kwa matumizi ya nyumbani na kunywesha mifugo wao.

“Miti iliyokuwa kijani kibichi sasa imekauka. Hatujui tutatoa wapi lishe ya mifugo,” akasema.

Wadudu hao walianza kuongezeka kwa wingi punde baada ya msimu wa mvua mwaka uliopita.

Wafugaji sasa wanalazimika kuhamia maeneo ya mbali kutafuta maji na lishe.

Katika Kaunti ya Baringo, kuna hofu katika vijijii kadhaa vilivyo katika Wadi ya Tirioko, eneobunge la Tiaty baada ya kuvamiwa na nzige.

Kwa mujibu wa wakazi, nzige walionekana katika maeneo ya Kamrio, Kapunyany, Chepkererat, Kamokol, Chepakana Hills, Tiaty Hills katika Wadi a Titioko, na eneo la Maron lililo Kerio Valley.

Cheposirwo Lonoki, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kamrio alisema nzige walionekana eneo hilo Jumamosi jioni kabla kuelekea Kamokol Hills Jumapili jioni.