Michezo

GORP FC yalenga kusajili matokeo mazuri

February 5th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Grain of Rice Project (GORP FC) inapania kujituma kwenye mechi za Kundi B Ligi ya Kaunti ya Nairobi West muhula huu.

Wachezaji hao wanaoshiriki ngarambe hiyo kwa mara ya pili wanataka kupambana kufa kupona ili kutwaa tiketi ya kupanda ngazi kushiriki kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL) msimu ujao.

Kocha wake, John Orosia anasema walianza kampeni zao vibaya lakini endapo wataendelea kufanya vyema hawana sababu ya kutomaliza kileleni na kunasa tiketi ya kusonga mbele.

“Katika mpango mzima hatuna la ziada mbali tumekusudia kukabili wapinzani wetu kiume kuhakikisha tunashinda mechi zetu zote,” anasema na kuongeza kuwa kamwe hawawezi kudharau wapinzani wao maana soka halina heshima.

Anadokeza kuwa kwa sasa hawana changamoto nyingi ilivyokuwa msimu uliopita walikomaliza nafasi ya nne katika jedwali la kipute hicho.

Anadai kipindi hicho hawakuwa na uwanja wa kufanyia mazoezi pia usafiri ulikuwa tatizo.

Kwa sasa chipukizi hao hutumia uwanja wa Laini Saba, Kibera kufanyia mazoezi pia wapo wahisani wamejitolea kuwasaidia kwa usafiri wanaoenda kushiriki za mechi kinyang’anyiro hicho ugenini.

”Ninaamini vijana wangu wameiva vizuri kuvuruga wapinzani wao na kumaliza kati ya nafasi mbili bora lakini sana sana kuibuka mabingwa ili kufuzu kupandishwa daraja. Raundi hii sio kama msimu uliyopita ingawa Shule zikifunguliwa wakati mwingine hukosa huduma za baadhi ya wachezaji wangu wazuri.”

Kocha huyo anasema timu zote zimejipanga kuonyesha ubabe wake kwenye harakati za kufukuzia ubingwa wa taji la muhula huu. GORP FC chini ya nahodha, Javanson Nabiswa na naibu wake, Erick Veke ni kati ya vikosi vinavyotifua kivumbi kikali kwenye kampeni za migarazano ya msimu huu.

GORP FC inakamata nne bora kwenye jedwali kwa kuzoa alama 13 baada ya kusakata mechi saba ambapo imeshinda nne, kutoka nguvu sawa mara moja na kudondosha patashika mbili.

Red Carpet inaongoza kwa kusajili pointi 18, mbili mbele ya Karura Green FC baada ya kupiga mechi nane na sita mtawalia. Nayo Gachie Soccer Kwa kufikisha alama 14 pia kucheza mechi saba inafunga tatu bora.

Yakuza vipaji

GORP iliyobuniwa mwaka 2017 inaorodheshwa kati ya vikosi vinavyoendelea kukuza wachezaji chipukizi hapa nchini.

Pia inajivunia kukuza talanta za wanasoka kadhaa ambao wanaochezea baadhi ya timu zinazoshiriki soka la ligi zingine. Imekuza mchezaji mmoja, Nicholas Omondi ambaye husakatia Gor Mahia ya Ligi Kuu ya KPL.

Pia wapo Mathew Omondi, Isaac Kimonyi na Kelvin ‘Olunga’ Omondi (Kibera Saints), Joseph Wanyiri, Martin Odhiambo na Geoffrey Karanja (Kemri) ambazo hushiriki kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL).