Makala

Nubian Flame: Mwanamuziki aliyekuwa na ndoto ya kuwa mpishi hodari

February 12th, 2020 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

ALIANZA uimbaji mnamo mwaka 2015 baada ya kupigana na hamu ya kuingia katika sanaa hiyo ambayo anaifanya kama kazi yake ya kila siku.

Abdul Musa Issa, ambaye anajulikana kama Nubian Flame kwa jina la kisanii, alizaliwa na kulelewa katika maeneo duni Nairobi.

Alikuwa na ndoto ya kuwa mpishi hodari alipokuwa akikua.

Ndoto yake ilitokana na uhusiano wa karibu na mamake ambaye alipenda upishi sana.

“Katika sherehe za kuzaliwa nilipofikisha umri wa miaka 12, mamangu alinizawadi jiko la kisasa la upishi na nilipokuwa na umri wa miaka 14, nilikuwa tayari najua kwa kiwango kikubwa upishi wote,” akasema Musa.

Hata hivyo, ndoto ya Musa ilibadilika baada ya mjomba wake kumzawadi na kanda ya nyibo za mtindo wa reggae.

Mjomba wake alienda sana nyimbo za aina hiyo nah ii ilichangia pakubwa katika kuupenda muziki wa reggae.

Baada ya kukamilisha masomo yake, Musa alijitoza katika sanaa hiyo na kuanza kurekodi nyimbo mtindo aina ya reggae.

“Naupenda sana muziki wa aina ya reggae kwani naweza kujieleza vizuri kupitia sanaa hiyo,” akasema Musa.

Kufikia sasa ana albamu moja ya nyimbo za reggae huku akijiandaa kuizindua ya pili mwaka huu 2020.

Baadhi ya hafla ambazo amehudhuria na kuonyesha kipaji chake cha muziki kwa kutumbuiza ni pamoja na Reggae Revolution, The Go Down, Reggae in The Sun, Alchemist Bar, na Nyama Mama Rest.