Habari MsetoSiasa

Bunge laidhinisha Mutahi Kagwe na Betty Maina kuwa mawaziri

February 26th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE Jumatano waliidhinisha uteuzi wa aliyekuwa Seneti wa Nyeri Mutahi Kagwe na Betty Maina kuwa mawaziri wa Afya na Viwanda, mtawalia.

Wawili hao waliteuliwa katika baraza la mawaziri, katika mabadiliko yaliyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Januari 14, 2020.

Bw Kagwe sasa ataapishwa rasmi ili aanze kuchapa kazi kama Waziri wa Afya baada ya Bi Sicily Kariuki kuhamishwa hadi Wizara ya Maji.

Na Bi Maina, ambaye awali alihudumu kama Katibu wa Wizara ya Ustawi wa Viwanda, Biashara na UjasiriaMali sasa ataapishwa kutwaa uongozi wa wizara hiyo.

Bw Kagwe ataingia afisini wakati ambapo Kenya iweka tahadhari kubwa baada ya mkurupuko wa Homa ya China kuripitiwa nchini China Desemba mwaka jana. Kufikia sasa, ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya corona umeangamizi takriban watu 2,200 wamefariki nchini China huku zaidi ya watu 70,000 wakiambuzwa virusi hivyo, maarufu kama, Covid -19.

Vile vile, Bw Kagwe anaingia afisini wakati ambapo Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) imeelekezewa lawama nyingi baada ya madai kuchipuza kwamba haitekelezi majukumu yake ipasavyo.

Alipokuwa akipigwa msasa na wabunge wiki jana, Bw Kagwe aliahidi kutekeleza mageuzi makubwa katika hazina hiyo, hatua ya mwanzo ikiwa na kuteua Afisa Mkuu Mtendaji mpya.

Bw Nicodemus Odongo, amekuwa akishikilia wadhifa huo kama kaimu Afisa Mkuu tangu Aprili 2018 Bw Geoffrey Mwangi alipoondolewa mamlakani baada ya kushtakiwa kwa sakata ya ufisadi ya kima cha Sh2 bilioni.

Wateule wengine ambo majina yao yaliidhinishwa na wabunge ni Julius Ouma Jwan aliyeteuliwa Katibu wa Idara ya Mafunzo ya Kiufundi, Balozi Simon Nabukwesi, Katibu wa Idara ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Utafiti na Enosh Onyango Momanyi kama katibu wa Idara ya Mipango ya Miji.