Habari

Feri mpya yawasili Mombasa

April 25th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

FERI mpya; MV Safari iliyotengenezwa nchini Uturuki na iliyogharimu serikali Sh1 bilioni imewasili nchini baada ya kutia nanga katika kivuko cha Likoni mjini Mombasa leo Jumamosi.

Mkurugenzi wa Shirika la Feri Nchini (KFS) Bw Bakari Gowa amesema kwamba MV Safari imeundwa kama feri ya MV Jambo ambayo ni ya kisasa.

MV Safari ina uwezo wa kuwavusha watu 1039 pamoja na wengine 12 wenye ulemavu na magari 54 kila awamu ya safari.

Bw Gowa hata hivyo amesema kwamba wakati huu ambapo serikali inaendelea kukumbwa na janga la Covid-19 MV Safari itabeba abiria 1,000 pekee ili kutekeleza sheria ya watu kutokaribiana sana.

“Feri hiyo ilitarajiwa kutia nanga Ijumaa jioni baada ya kukaguliwa ila haikuwezekana,” amesema Bw Gowa.

Miaka minne iliyopita serikali iliipa Kampuni ya Ozota iliyo Uturuki kandarasi ya kuziunda feri; MV Jambo na MV Safari ambapo MV Jambo ilikuwa ya kwanza kuwasilishwa humu nchini mwaka 2017.

Jumla ya Sh2.51 bilioni zilitengwa kufanikisha ununuzi wa feri hizo mbili.

Zaidi ya watu elfu mia tatu na hamsini na magari 6,000 hutumia kivuko hicho kila siku.

Tangu mwaka wa 1990 feri za MV Nyayo, MV Kilindini na MV Harambee zimekuwa zikitumiwa kuwavusha watu katika kivuko hicho na licha ya muda wake wa kuhudumu ambao ni miaka 25 kukamilika, zimekuwa zikiendelea kutumiwa.

Mwaka 2019 serikali ilitoa amri ya kusitishwa feri hizo kuhudumu baada ya moja kusababisha ajali ya mama na mwanawe aliyekuwa na umri wa miaka minne.

MV Likoni na MV Kwale ambazo pia zimekuwa zikitumiwa katika kivuko hicho, zilizinduliwa mwaka 2010.