Michezo

Kenya yatenga mamilioni kufanikisha vita dhidi ya pufya

May 17th, 2020 2 min read

GEOFFREY ANENE na MASHIRIKA

KENYA imetenga Sh17 milioni kufanikisha vita dhidi ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli kwa timu ya taifa itakayoshiriki Michezo ya Olimpiki 2020 jijini Tokyo nchini Japan mnamo Julai 23 hadi Agosti 8 mwaka 2021. Michezo hiyo iliahirishwa kutoka mwaka 2020 hadi 2021 kutokana ana janga la virusi vya corona.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua, likimnukuu Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Kukabiliana na matumizi ya pufya nchini Kenya (ADAK) Japhter Rugut, fedha hizo ni sehemu ya mpango wa wa kushinda vita dhidi ya uovu huo, ambao umeweka Wakenya, hasa wanariadha, katika hatari kubwa ya kupigwa marufuku kushiriki na hata Kenya kuandaa mashindano ya kimataifa.

Tangu mwaka 2012, zaidi ya Wakenya 60 wamepigwa marufuku kushiriki riadha baada ya kupatikana na hatia ya ‘kula dawa’ haramu ili kupata mafanikio mashindanoni.

Baadhi ya Wakenya, ambao wanatumikia marufuku ya kati ya miaka minne na minane kwa kupatikana wakitumia njia hiyo ya mkato kupata ufanisi ni bingwa wa mbio za kilomita 42 kwenye Olimpiki 2016 Jemimah Sumgong, bingwa wa London Marathon 2017 Daniel Wanjiru na bingwa wa zamani wa Olimpiki na Dunia wa mbio za mita 1,500 Asbel Kiprop.

“Tuna bajeti ya kufanikisha vita dhidi ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli kwenye michezo yetu. Kwa sasa, naamini tunashinda vita hivi, ingawa sidhani kama tatizo hili litawahi kuondolewa kabisa,” alisema Rugut katika mahojiano na Xinhua mnamo Mei 16 kabla ya kufichua kuwa ADAK imetengea programu ya kukabiliana na watumiaji wa dawa hizo dola 170, 000 za Marekani, ambayo ni Sh17 milioni za Kenya. Rugut alifichulia kituo hicho kuwa ADAK ilitumia Sh278,397,080 kwa shughuli sawa na hiyo wakati wa Riadha za Dunia 2019 zilizofanyika jijini Doha nchini Qatar.

ADAK, Rugut alisema, imefanya vipimo 4, 116 katika kipindi cha miaka minne. Kutoka orodha hiyo, sampuli 3, 552 zimekuwa za mkojo na 545 za damu. Shughuli hiyo ya kupima wanamichezo wa Kenya imeshuhudia 120 wakinyakwa upande na sheria, huku baadhi wakiadhibiwa kwa kuzuiwa kushiriki mashindano.

Hata hivyo, Xinhua inasema kuwa Shirikisho la Riadha Duniani (WA) lilikiri juma moja lililopita kuwa linakabiliwa na changamoto kubwa kukabiliana na uovu wa kutumia dawa zilizoharamishwa michezoni kwa sababu ya vikwazo vya usafiri wakati huu wa janga la corona kote ulimwenguni.

Kenya iko katika orodha ya mataifa yanayomulikwa zaidi ya Shirika la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli pamoja na Ethiopia, Ukraine, Belarus, Nigeria, Bahrain na Nigeria.