Michezo

Mwanatenisi Roger Federer sasa ndiye mwanamichezo anayelipwa fedha nyingi zaidi duniani

May 30th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

ROGER Federer, 38, amekuwa mwanatenisi wa kwanza kuongoza orodha ya Forbes ya wachezaji wanaodumishwa kwa mishahara ya juu zaidi duniani baada ya kumpiku mwanasoka Lionel Messi wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina.

Federer ambaye ni mzawa wa Uswisi, alisonga juu kwa hatua nne zaidi baada ya kutia kapuni kima cha Sh12 bilioni mwaka jana. Takriban Sh11.3 bilioni za mapato hayo zilitokana Federer kuwa balozi wa mauzo ya bidhaa za kampuni mbalimbali.

Mgongo wa Federer kwa sasa unasomwa kwa karibu na Cristiano Ronaldo (Sh11.9 bilioni), Messi (Sh11.7 bilioni) na Neymar (Sh10.8 bilioni).

Mwanavikapu maarufu mzawa wa Amerika, LeBron James (Sh10 bilioni) anakamilisha orodha ya tano-bora.

Mwanamasumbwi Tyson Fury ndiye Mwingereza anayelipwa mshahara wa juu zaidi ulimwenguni. Anashikilia nafasi ya 11 duniani kwa kima cha Sh6.5 bilioni.

Bingwa wa dunia katika mbio za magari ya Langalanga (Formula 1), Lewis Hamilton anashikilia nafasi ya 13 kwa mapato ya takriban Sh6.1 bilioni kwa mwaka.

Mwanatenisi Naomi Osaka wa Japan ndiye mwanamichezo wa kike anayelipwa mshahara mnono zaidi duniani. Anashikilia nafasi ya 29 kwa ujumla.

“Janga la corona lililoathiriwa shughuli nyingi za michezo tangu mwaka jana lilitikisa kiwango cha mapato ya Ronaldo na Messi katika ulingo wa soka. Mlipuko wa virusi hivyo ulimpa Federer fursa ya kuzidisha urefu wa kina cha mifuko yake katika ulingo wa spoti na hatimaye akaibuka kileleni kwa mara ya kwanza,” akasema Kurt Badenhausen ambaye ni mhariri mzoefu wa Jarida la Forbes.

“Federer amakuwa kivutio kwa kampuni nyingi za utangazaji wa bidhaa na huduma kwa njia za kielektroniki. Mengi ya matangazo ambayo amekuwa akifanya tangu mwanzoni mwa 2019 yalimvunia ujira wa takriban Sh10 bilioni mwaka huo,” akaongeza Badenhausen.

Wiki jana, Osaka, 22, ambaye ni bingwa mara mbili wa taji la Grand Slam, alikomesha ukiritimba wa miaka minne wa Serena Williams wa kuwa mwanamichezo wa kike anayelipwa vyema zaidi duniani baada kufichuliwa kwamba alijizolea jumla ya Sh4.3 bilioni. Fedha hizo zilizidi zile alizopata Serena, 38, kwa takriban Sh161 milioni.