Habari

Raha yake kuua wanawake?

June 30th, 2020 3 min read

STEVE NJUGUNA na WAIKWA MAINA

MAHAKAMA mjini Nyahururu imewaruhusu polisi kumzuilia kwa siku 21 mwanamume anayedaiwa kuhusika katika msururu wa mauaji ya wanawake na watoto.

Jaribio la hivi punde zaidi la mauaji ni la Jumapili usiku ambapo Bi Phylis Wanjiru alinusurika kifo baada ya mshukiwa huyo kuchimba handaki na kufanikiwa kuingia kwenye kuchumba cha malazi ambapo Wanjiru alikuwa amelala na wanawe.

Kufikia Jumatatu, bado Wanjiru alikuwa ameshtuka pakubwa.

Mshukiwa Jassan Kariuki, 27, ambaye alikamatwa Jumapili, anaaminika kushiriki katika visa vingi vya mauaji na wizi wa mabavu katika eneo la Nyandarua Magharibi.

“Sikuwa na uhasama wowote naye. Nilisikia kama kwamba mtu anachimbachimba nyuma ya nyumba yangu usiku kisha akafanikiwa kuingia kabla niitishe usaidizi,” akaeleza Bi Njeri.

Alisema mshukiwa alimkuta kitandani akiwa chonjo, akamwita mshukiwa kwa jina lakini alimrukia akaanza kumnyonga.

“Ilinibidi nijipiganie huku nikipiga mayowe. Lakini alifanikiwa kutoroka. Majirani walinishauri niripoti kwa polisi. Alikuwa ametishia kurudi kuniua pamoja na watoto wangu kama ningemtaja kwa mtu yeyote,” akasema.

Mshukiwa alikuwa akiishi katika chumba kidogo kilichojengwa kwa mbao nyumbani kwa mamake, akiwa na bafu ambayo imejengwa kwa nailoni bila milango.

Na jana, Sajini Peter Mukangai aliiomba mahakama kuwapa polisi muda kufanya uchunguzi zaidi, kwa kuwa wanaamini kuwa mshukiwa amekuwa akishiriki kwenye visa vingine vingi vya mauaji eneo hilo.

Mshukiwa huyo alikamatwa katika eneo la Nyakariang’a, eneobunge la Ol Joro Orok, baada ya jaribio la wizi wa mabavu na mauaji kutibuka.

Kulingana na polisi, mshukiwa alikuwa amechimba handaki ili kuvamia nyumba ambayo mwanamke aliyekusudia kumshambulia alikuwa amelala na wanawe.

“Kutokana na muda mfupi uliopo tangu tulipomkamata na tulipomfikisha mahakamani, hatukuweza kuandikisha taarifa kutoka kwa mshukiwa mwenyewe wala walalamishi. Tunachunguza msururu wa visa vya uhalifu ambavyo vimefanyika katika eneo la Nyandarua Magharibi kati ya Desemba 2018 hadi sasa,” akasema Bw Mukangai mbele ya Hakimu Mkuu Charles Obulutsa.

Mahakama iliambiwa kwamba, mshukiwa anatuhumiwa kushiriki kwenye mauaji ya watu wanne kwa sasa, wanaojumuisha wanawake na watoto. Wanne hao wameuliwa eneo hilo katika hali ya kutatanisha.

“Tunapanga kumfungulia mashtaka zaidi. Ni kwa hilo ambapo tunaomba muda zaidi ili kuendesha uchunguzi wetu. Mashtaka hayo yatajumuisha mauaji, wizi wa mabavu kati ya mengine. Tunaamini kuna washukiwa wengine ambao amekuwa akishirikiana nao na bado hawajakamatwa,” akasema.

Alipoulizwa na hakimu ikiwa alielewa polisi alivyoiambia mahakama, aliitikia tu kwa kutikisa kichwa.

Akikubali ombi hilo, hakimu alisema madai hayo ni yenye uzito, hivyo inawahitaji polisi kufanya uchunguzi wa kina.

Aliagiza mshukiwa kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Ol Joro Orok hadi Julai 13, wakati kesi hiyo itakapotajwa tena.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Ol Joro Orok, Bw Wanyama Nyongesa alisema wapelelezi wanachunguza simu sita zilizopatikana nyumbani kwake ili kubainisha kama alikuwa akitenda uhalifu peke yake.

“Tumechunguza upya mauaji mengine na tukatambua yote yalitendwa kwa njia zinazofanana na yote yalitokea mwezi ukikaribia kuisha. Tulipata pia sarafu za Uganda, kumaanisha hili si jambo la kufanyiwa mzaha,” akasema.

Miongoni mwa silaha zilizopatikana nyumbani kwake ni panga, kisu, msumeno, shoka na jembe.

Nyumbani kwa mshukiwa katika kijiji cha Nyakarianga, Kaunti ya Nyandarua, wanakijiji walidai mwanamume huyo alifahamika kuwa mhalifu kwa muda mrefu na wengi humwogopa sana.

Mamake ambaye alionekana kukerwa sana na mienendo yake, alikataa kusema mengi lakini akaeleza anafurahi mwanawe amekamatwa na polisi.

“Wakati mwingi hatukujua alikuwa wapi kwa sababu huwa hatumwoni nyumbani. Yeye ni mtu mzima, hatuwezi kudhibiti mienendo yake. Lakini tulikuwa tumepokea malalamishi kuhusu vitendo vyake vya uhalifu kutoka kwa majirani,” akasema.

Sawa na polisi, majirani walisema wanashuku alihusika katika mauaji mengi ambayo yametokea tangu alipoondoka gerezani mwaka uliopita.

“Alizaliwa na kulelewa katika kijiji hiki na alikuwa muumini wa dini sana lakini tabia zake zilianza kubadilika akiwa darasa la tano. Alihangaisha watoto na mara nyingi akalaumiwa kwa wizi wa kuku na mbuzi. Alikuwa mbaya zaidi baada ya darasa la nane, lakini sote tulidhani angebadilika baadaye,” akasema mmoja wa majirani.

Jirani mwingine ambaye alisoma naye shule moja, alisema ana bahati alikamatwa na polisi kwani hivi karibuni angewaua na raia.

“Hatuelewi kwa nini alilenga wanawake na watoto pekee. Polisi pia walifahamu uhalifu wake, lakini haieleweki kwa nini ilichukua muda mrefu kabla akamatwe,” akasema.