Habari MsetoSiasa

Sitabomoa makaburi ya Waislamu, Gavana aahidi

July 19th, 2020 1 min read

Na RUSHDIE OUDIA

GAVANA wa Kisumu, Prof Anyang Nyong’o amewahakikishia waumini wa dini ya Kiislamu kwamba makaburi yao mjini humo hayataharibiwa katika mpango wa kustawisha jiji.

Baadhi ya viongozi wa Kiislamu walikuwa wamepanga kukutana na gavana huyo ili walalamikie mipango ya kuvuruga makaburi hayo ambayo yamekuwepo kwa miaka mingi.

Prof Nyong’o alisema makaburi hayo ambayo yako karibu na uwanja wa gofu wa Nyanza, na kaunti haina mpango wa kugusa eneo lolote la kihistoria endapo ubomoaji utahitajika katika mpango wa kunadhifisha ufuo wa Ziwa Victoria.

Akizungumza katika mahojiano ya redio Ijumaa, gavana huyo alisema ijapokuwa katika miaka ijayo kutahitajika eneo jingine la makaburi ya Waislamu katika sehemu nyingine ya mji, makaburi yanayotumiwa sasa yataendelea kuwepo.

‘Makaburi hayo yana umuhimu mkubwa wa kidini, kihisia na kihistoria kwa ndugu na dada zetu Waislamu kwa hivyo hatuwezi kuyagusa,’ akaeleza.Jana, Prof Nyong’o aliwahakikishia wakazi na waekezaji Kisumu kwamba mpango wa kustawisha mji huo utatekelezwa kwa njia ambayo itaepusha uharbifu mkubwa wa uchumi na makazi ya watu.

Mpango huo ulikuwa umeanza Julai 2019 na utakaodumu kwa miaka mitano ulianza kwa upanuzi wa Bandari ya Kisumu. ambapo majengo kadhaa ya kibiashara yalibomolewa.

Prof Nyong’o alisema lengo lake kuu ni kuhakikisha Kisumu ni jiji safi lenye mpango wa ujenzi wa kuvutia.Kupitia kwa washauri wake, kaunti hiyo ilianzisha mashauriano na umma.

‘Tunahusisha kila mtu katika mpango huu muhimu na ninatoa wito kwa wakazi wa Kisumu wajitokeze ili wafanyie utathmini sera na mikakati iliyopendekezwa,’ akasema gavana.