Habari Mseto

Baadhi ya Wajomvu waandamana Mombasa malalamiko yakiwa unyakuzi wa vipande vya ardhi

July 20th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

BAADHI ya watu kutoka kwa jamii ya Wajomvu mjini Mombasa wameandamana Jumatatu wakipinga unyakuzi wa vipande vya ardhi waliosema unaoendelea katika eneo lao.

Jamii hiyo ambayo ni miongoni mwa jamii za kwanza kutua katika mji wa Mombasa, inadai ilipokonywa kipande cha ardhi na wageni wanaotoa hongo ili kupata hatimiliki.

Wakazi hao ambao ni zaidi ya watu 10,000 na wanaoishi eneo la Jomvu Kuu waliipa serikali makataa ya siku 10 kuhakikisha wanarudishiwa kipande chao cha ardhi.

“Tumekuwa tukiishi hapa kwa zaidi ya miaka 800 ikizingatiwa akina babu zetu ndio walishika eneo hili na hata makaburi yao yako sehemu hii. Sasa tunashangaa kuona wageni kutuka maeneo mengine wakidai umiliki wa kipande hiki cha ardhi,” akasema Bw Salim Mwidani mzee wa mtaa huo.

Bw Mwidani alisema kwa sasa wamesalia na hekari sita pekee, huku wageni wakimiliki sehemu kubwa ya eneo hilo.

Walisema japo waliwasilisha malalamiko yao kwa senata wa Mombasa Mohammed Faki na kamishna Bw Gilbert Kitiyo hawajapata suluhu la tatizo hilo.

“Tulipomfuata kamishna alituagiza kwenda kortini kusitisha shughuli za ujenzi katika sehemu hii kisha tupeleke malalamishi yetu mahakamani,” akasema Bw Mwidani.

Bw Salim Mwidani (kushoto) na mwenye shati la waridi ni Bw Ahmed Kombo. Picha/ Mishi Gongo

Msemaji wa jamii hiyo Bw Ahmed Kombo alisema ardhi iliyonyakuliwa inawazuia wao kuendeleza shughuli zao za uvuvi na hata kuzika jamii zao.

“Sehemu iliyokuwa ni maziara sasa ni ardhi ya kibinafsi haturuhusiwi kupita haliyakuwa sisi ndiyo wamiliki,” akasema Bw Kombo.

Mkazi katika eneo hilo Bw Mwinyiusi alisema kuwa wageni hao wanatumia maafisa wa polisi kuwahangaisha wakazi kila mara wanapojaribu kudai haki yao.

“Tukijaribu kujitetea tunatumiwa maafisa wa polisi kutukamata na kutuhangaisha, hatutakubali ardhi yetu kunyakuliwa,” akasema.

Mkazi mwingine Bi Fatuma Mwinyi alisema kwa sasa wanalazimika kufinyana katika nyumba ndogo kwa kukosa nafasi ya kujenga.