Michezo

Villarreal na Real Madrid nguvu sawa kwenye La Liga

November 22nd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walipoteza fursa ya kupunguza mwanya wa alama kati yao na viongozi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Real Sociedad, hadi pointi moja baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 kutoka kwa Villarreal mnamo Novemba 21, 2020.

Mariano Diaz aliwaweka Real uongozini kupitia bao la kichwa katika dakika ya pili ya kipindi cha kwanza kabla ya Villarreal kusawazisha kupitia penalti ya Gerard Moreno baada ya Samuel Chukwueze kuchezewa visivyo ndani ya kijisanduku.

Moreno alipoteza fursa nzuri ya kuwavunia Villarreal ya kocha Unai Emery alama zote tatu mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kombora aliloelekeza langoni pa wapinzani wao kuzuiliwa na beki Raphael Varane.

Ushindi kwa Villarreal katika mechi hiyo ungaliwakweza hadi kileleni mwa jedwali la La Liga. Hata hivyo, walisalia katika nafasi ya tatu kwa alama 19, mbili zaidi kuliko mabingwa watetezi Real Madrid.

Mwishowe ilikuwa alama moja muhimu kwa Real ambao walikosa idadi kubwa ya wanasoka tegemeo kutokana na majeraha.

MATOKEO YA LA LIGA (Novemba 21, 2020):

Villarreal 1-1 Real Madrid

Atletico Madrid 1-0 Barcelona

Levante 1-1 Elche

Sevilla 4-2 Celta Vigo