Habari

Vuguvugu la Linda Katiba kutumia mbinu tatu kupinga marekebisho ya katiba kupitia BBI

November 29th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Narc Kenya Martha Karua na mwanauchumi David Ndii wamesema watawasilisha kesi mahakamani kupinga mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) wakisema ni kinyume cha Katiba.

Wamesema Katiba ya 2010 haina dosari yoyote ni kile kinachohitajika sasa ni kufanikisha utelelezwaji wake kikamilifu wala sio kuifanyia marekebisho kwa njia ambayo ‘inaendeleza utawala wa rais mwenye mamlaka zaidi na kuwabebesha Wakenya mzigo kupitia kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za utawala zikiwemo zile za bungeni.”

Chini ya mwavuli wa vuguvugu la Linda Katiba, wawili hao kwa ushirikiana na wanaharakati wa kutetea haki Boniface Mwangi na Jerutich Sii wamesema Jumapili  kuwa watapinga mchakato huo pia kupitia maandamano na amani na uhamasisho wa umma.

“Mchakato wa marekebisho kupitia BBI hautokani na shinikizo kutoka kwa wananchi bali watu wawili ambao ni Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga. Kwa hivyo, wananchi hawafai kushirikishwa katika mchakato huu na kufanya hivyo ni kinyume cha Katiba,” Bi Karua ambaye ni Wakili Mkuu (Senior Counsel) amewaambia wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi, Jumapili.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa marekebisho ya katiba ambayo huidhinishwa na wananchi kupitia kura ya maamuzi huo ni yale ambayo yamependekezwa na wao wenyewe, kulingana na kipengele cha 257 cha Katiba.

“Huu mchakato ulianzishwa na watu wawili baada ya wao kusalimiana mnamo Machi 9, 2018. Haukupendekezwa na Wakenya na hivyo yale yote yanayoendelea sasa ikiwemo ukusanyaji wa sahihi za Wakenya ni harakati zilizo kinyume cha Katiba,” akasema Bi Karua ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Gichugu kwa miaka 20 na Waziri wa Haki na Masuala ya Kikatiba.

Martha Karua akiongea na wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi, Novemba 29, 2020, kupinga marekebisho ya katiba kupitia BBI. Chini ya mwavuli wa vuguvugu la ‘Linda Katiba’ Karua na wenzake wamesisitiza wataenda kortini kupinga ukusanyaji sahihi na mchakato mzima wa marekebisho ya katiba kupitia BBI. Wanaharakati wengine ambao ni wanachama wa vuguvugu hilo ni pamoja na mwanauchumi David Ndii, mwaharakati wa kutetea haki Boniface Mwangi, mtetezi wa haki za akina mama Daisy Amdany na mwaharakati Bi Jerutich Seii. Picha/ Charles Wasonga

Kwa upande wake Bw Ndii amesema kushirikishwa kwa machifu na maafisa wengine wa utawala katika shughuli ya ukusanyaji sahihi za kuidhinisha mswada wa marekebisho ya Katiba ni ishara tosha kwamba huu ni “mradi wa serikali” wala sio wa wananchi.

“Tumepata habari kwamba machifu wanalazimishwa na kutishwa wawashirikishe wananchi kutia saini zao kwa mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia BBI. Ni sawa na kurejeshwa kwa utawala wa kiimla wa KANU ambapo utawala wa mkoa ulitumiwa kuendeleza urais wa kifalme,” akasema Bw Ndii ambaye zamani alikuwa mwandani wa Bw Odinga.

Akaongeza: “Tunawaomba Wakenya kukataa mtindo huu wa matumizi mabaya ya mamlaka na wafichue, kupitia mitandao ya kijamii, visa ambapo machifu wanatumiwa kuendeleza ukusanyaji sahihi.”

Amekariri kuwa msimamo wao kama vuguvugu la “Linda Katiba” ni kwamba Katiba ya sasa ni nzuri na malalamishi kuhusu kasoro zinazosababisha ghasia kila baada ya uchaguzi yanaweza kushughulikiwa kupitia mapendekezo ya Ripoti ya Kriegler.

“Masuala mengine kuhusu kasoro katika utawala kama vile ubaguzi katika uteuzi wa maafisa wakuu serikalini, ukabila na kukithiri kwa ufisadi miongoni mwa maafisa wa serikali yanaweza kushughulikiwa kupitia utekelezaji wa vipengele vya 10 na 86 vya Katiba,” akasema Bw Ndii.

Amesema BBI ni zao la makosa yaliyotokea katika mfumo wa uchaguzi, ambayo yanaweza kurekebishwa bila marekebisho ya Katiba.

Bw Mwangi naye amemsuta Bw Odinga kwa kuwatelekeza wafuasi wake katika safari ya Canaan kwa “kugeuka na kurejea Misri”.

“Inashangaza kuwa Raila amegeuka msaliti mkubwa kwa kushirikiana na Uhuru kuhujumu mageuzi ambayo amepigania kwa miaka mingi. Amekatiza safari ya Canaan na sasa amerejea kwa Firauni kule Misri kuendeleza sera za kuwakandamiza raia,” akasema.