Uhuru ataweza Raila na Ruto?

Uhuru ataweza Raila na Ruto?

Na BENSON MATHEKA

SIKU moja baada ya viongozi wa chama cha ODM kulalama kuwa kuna njama ya Rais Uhuru Kenyatta kumsaliti kiongozi wao Bw Raila Odinga, maswali yameibuka kuhusu iwapo Rais atafanikiwa kumlemea waziri huyo mkuu wa zamani pamoja na Naibu Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2022.

Mnamo Jumamosi, Seneta wa Siaya, Bw James Orengo alidai kuwa baadhi ya maafisa wa serikali ambao hakuwataja majina wanapanga njama za kuhujumu ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga wakilenga kumzuia kushinda urais ilivyofanyika kwenye uchaguzi wa 2007, 2013 na 2017.

Bw Odinga na washirika wake wanaamini kwamba alishinda urais kwenye chaguzi hizo lakini akaibiwa kura, juhudi ambazo wanadai ziliongozwa na watu waliokuwa na ushawishi serikalini.

Pamezuka minong’ono kuwa iwapo Rais Uhuru atamkwepa Bw Raila katika uchaguzi mkuu ujao, pana uwezekano mkubwa wa ama kinara huyo wa chama cha Chungwa kuungana na Dkt Ruto au kila mmoja kati yao awanie kivyake kupingana na chaguo la Bw Uhuru.

Duru zinasema kwamba Rais Kenyatta huenda akaubariki muungano unaonukia kati ya kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, mwenyekiti wa chama cha Kanu, Bw Gideon Moi, Bw Kalonzo Musyoka wa Wiper na Moses Wetangula wa chama cha Ford Kenya.

Wanne hao waliungana katika kampeni za uchaguzi mdogo wa maeneobunge ya Matungu, Kaunti ya Kakamega ambao Peter Nabulindo wa ANC alimshinda David Were wa ODM na Kabuchai ambako Majimbo Kalasinga wa Ford Kenya alishinda.

Duru zinasema kwamba wandani wa Bw Odinga wanaamini kwamba watu wenye ushawishi serikalini walisaidia kuangushwa kwa mwaniaji wa chama cha ODM katika uchaguzi mdogo wa Matungu ili kumsawiri kiongozi wa chama chao kama aliyepungua umaarufu.

Mudavadi, Kalonzo na Wetangula ambao walikuwa washirika wa Bw Odinga kwenye muungano wa NASA katika uchaguzi mkuu wa 2017 wameashiria kuwa wataungana na Moi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 bila Raila. Mshirika mmoja wa Bw Odinga alisema kuna mipango ya Rais Kenyatta kumteua mwanasiasa kutoka Mlima Kenya kuungana na wanne hao huku yeye Rais akiwa mdhamini wao mkuu.

Ikiwa madai ya ODM ni ya kweli, huenda mabadiliko makubwa ya kisiasa yakashuhudiwa kabla au baada ya kura ya maamuzi. Wadadisi wanasema iwapo atamtema Bw Odinga, Rais Kenyatta atakuwa ameongeza mahasimu wake kisiasa ikizingatiwa kuwa uhusiano wake na Dkt Ruto umeingia doa.

“Siasa za usaliti, kutumiwa na kuzimwa si ngeni nchini Kenya na chanzo chake huwa si viongozi walio mamlakani bali huwa ni wanaofaidika na uongozi wao. Hapa ninazungumzia wanaolinda mamlaka na huwa wana nguvu sana,” asema mdadisi wa siasa Geoffrey Kamwanah.

Kumtema Raila na kumuunga yeyote katika muungano wa Mudavadi, Kalonzo, Moi na Wetangula, kunaweza kuunganisha Bw Odinga na Dkt Ruto tena licha ya wawili hao kushambuliana kuhusu handisheki na mchakato wa kubadilisha katiba.

Wadadisi wanasema kwamba wawili hao wanaweza kuungana kumkabili adui mmoja au kila mmoja agombee kivyake wakielekeza mishale yao kwa Rais Kenyatta.

“Dkt Ruto alimsaidia Uhuru kuingia mamlakani lakini akamtema, Raila alimsaidia kumtema Ruto na kuongoza kwa utulivu katika kipindi chake cha pili. Bila shaka Uhuru atakuwa na wakati mgumu kuuza chaguo lake kwa kuwa ataonekana msaliti,“ aeleza Bw Kamwanah.

Hisia za wandani wa Bw Odinga na Dkt Ruto ni kuwa Rais Kenyatta aliwatumia kutimiza maslahi yao ya kisiasa na kuwagonganisha wasishirikiane kisiasa ili chaguo lake lisiwe na upinzani mkubwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Handisheki ilivunja chama cha Jubilee ambacho ilitarajiwa Dkt Ruto angetumia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao na muungano wa Nasa ambao uliipa Jubilee ushindani mkali chini ya Bw Odinga.

Hata hivyo, Dkt Ruto amefaulu kujenga chama cha United Democratic Alliance (UDA) kupitia kampeni yake ya hasla na umaarufu wake umeongezeka nchini ikiwemo ngome ya Rais Kenyatta ya Mlima Kenya.

Wadadisi wanasema kuwa Bw Odinga ni mwanasiasa mzoefu anayeweza kusambaratisha mipango ya Rais Kenyatta ukiwemo mchakato wa kubadilisha katiba wa BBI akihisi kwamba anahujumiwa.

Bw Raila alitarajiwa kuzungumzia tetesi hizo za kusalitiwa katika uwanja wa Kamukunji, Kibera, Nairobi, Jumapili lakini baadaye ikasemekana kuwa Ikulu iliingilia kati na kumshauri kutohudhuria huku suluhu ikitafutwa.

You can share this post!

DIMBA: Huyu chipukizi En-Nesyri anawindwa kama Mo’ Salah

UDAKU: Kipa De Gea raha tele kuangusha kimalaika