Hii hapa siri ya mbuzi kuzaa mapacha; kutoa maziwa mengi

Hii hapa siri ya mbuzi kuzaa mapacha; kutoa maziwa mengi

NA SAMMY WAWERU

NAIVAFRESH Goat Dairies, ni mradi wa ufugaji mbuzi wa maziwa eneo la Gituamba, Naivasha, kilomita tatu kutoka barabara kuu ya Nairobi – Nakuru, wenye mbuzi 120.

Kinachokukaribisha katika mazingira yake, ni sauti tofauti za wanyama hao wa nyumbani.

Makao yamejengwa kulingana na umri na hali ya mbuzi. Yakiwa yameinuliwa juu kiasi, kuna ya vibuli (wana wa mbuzi), waliozaa na wanaoendelea kunyonyesha.

Vilevile, yapo ya mbarika (mbuzi wa kike) na beberu. Samuel Njoroge, meneja wa mradi anasema mbinu hiyo ni mojawapo katika kufanikisha ufugaji wa mbuzi.

Huku maziwa ya wanyama hao yakiwa adimu nchini, mbuzi wa Naivafresh huzalisha wastani wa lita tatu kila siku, kwa kila mbuzi.

“Asubuhi, kila mbuzi huzalisha lita mbili na jioni moja,” Njoroge aelezea, akifichua kwamba mradi huo hufuga mbuzi aina ya Alpine wenye asili ya Ujerumani, Ufaransa na Uingereza.

Cha kushangaza, wengi huzaa mapacha, suala ambalo Njoroge anahoji mradi huo umegundua siri.

Idadi kubwa ya wafugaji wakidhania aina (breed) ya mbuzi na jeni (genes) ndiyo chanzo cha mapacha, mtaalamu huyu mwenye Digrii ya Masuala ya Sayansi kwenye mifugo kutoka Chuo Kikuu cha Egerton anasema siri ni malisho.

Si bora malisho, ila malisho bora kwa mbuzi wa kike. “Anaposhika mimba, anapaswa kulishwa chakula cha kutosha na chenye virutubisho faafu,” adokeza.

Aidha, mbuzi huzaa miezi mitano baada ya kujamiishwa na kutungwa mimba.

“Tunahakikisha wale wa kike tunawalisha nyasi aina ya Lucerne na Boma Rhodes, na chakula cha madukani. Kiwango cha Protini kipaswa kuwa cha juu,” anafafanua.

“Maji yawe kwa wingi na safi. Mbuzi akiwa mjamzito, anahitaji mapumziko ya kutosha.”

Kulingana naye, taratibu na vigezo hivyo ndivyo vimesaidia idadi kubwa ya mbuzi wa mradi huo kuzaa mapacha.

Joseph Mathenge, mfugaji hodari wa mbuzi wa maziwa Kiambu sawa na Njoroge anakiri nyasi zilizokauka ni chocheo la uzalishaji wa maziwa mengi.

“Maziwa huundwa kupitia maji wanayokunywa. Nyasi zilizokauka sawasawa huwapa motisha kuyanywa kwa wingi,” Mathenge asisitiza.

Isitoshe, Njoroge anahimiza haja ya Lucerne na Boma Rhodes kukuzwa kwa kuzingatia taratibu bora kitaalamu, pamoja na kuruhusu nyasi hizo kukomaa.

“Upanzi, matunzo na shughuli za mavuno zitiliwe maanani,” anashauri.

Kufanikisha utungishaji ujauzito, mdau huyu anasema wakati bora ni saa 12 baada ya mbarika kuonyesha dalili za kutaka dume.

“Hilo ni hakikisho la kushika mimba,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano katika mradi huo wa mbuzi, ambao husambaza maziwa sehemu mbalimbali nchini.

Alisema udumishaji wa hadhi ya juu ya usafi katika makao, kuzingatia ratiba ya chanjo na matibabu mbuzi wanapoonyesha udhaifu au dalili za maradhi husaidia kupunguza gharama ya ufugaji.

Homa ya Mapafu, Pink eye, Coccidiosis, Rift valley fever (RVF) na Pulpy kidney, ni miongoni mwa magonjwa hatari katika mbuzi. Vimelea ni minyoo, kupe na viroboto.

Njoroge anahimiza wafugaji kukumbatia mbuzi aina ya German Alpine (wenye rangi ya kahawia na michirizi mieusi kichwani na kwenye uti wa mgongo), British Alpine (mchanganyiko wa rangi nyeusi na nyeupe), na French Alpine (wa rangi nyeupe na kahawia).

“Kiwango chao cha uzalishaji wa maziwa ni cha juu,” asema.

Wateja wakuu wa Naivafresh Goat Dairies ni taasisi kama shule, hospitali, vituo vya afya, kampuni za kuongeza thamani na wakazi Naivasha na Kaunti ya Nakuru. Lita moja ya maziwa haipungui Sh200.

Mradi huo pia hutoa mafunzo ya ufugaji bora wa mbuzi wa maziwa, ukitoza ada ya Sh1, 000 kwa kila anayeutembelea kunoa bongo.

  • Tags

You can share this post!

Wakulima wa maembe hoi kampuni kukosa kununua zao

Tambua aina mpya ya mchele ya kusaidia utoshelevu wa chakula

T L