• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
OBARA: Mzaha huu wa viongozi hautamaliza majanga

OBARA: Mzaha huu wa viongozi hautamaliza majanga

Moto katika mtaa wa Kijiji, Langata, Kaunti ya Nairobi wawaacha wakazi kwa majonzi Januari 29, 2018. Picha/Hisani

Na VALENTINE OBARA

Kwa Muhtasari:

  • Maelezo ya viongozi kuhusu kukabiliana na majanga huleta matumaini tele kwa wananchi kwamba hao ni viongozi shupavu
  • Naibu Rais William Ruto, alifika katika eneo la mkasa wa moto  na kuelezea mikakati yake
  • Ahadi na mikakati inayotolewa wakati wa mikasa aina hii haziwezi kusaidia kwa njia yoyote
  • Wanasiasa hasa barani Afrika hupenda wananchi wawe maskini ndipo wafanikiwe kuwatumia jinsi watakavyo

WAKATI wowote janga la aina yoyote linapotokea nchini, viongozi hujitokeza na maelezo kuhusu mipango kabambe waliyo nayo kuzuia majanga katika siku za usoni.

Maelezo yao huleta matumaini tele kwa wananchi kwamba hao ni viongozi shupavu ambao wanastahili kuwa mamlakani kwani wana maono mazuri.

Hata hivyo, haya yote hutokomea punde waathiriwa wa janga husika wanaporejelea maisha yao ya kawaida kwani viongozi hao hukosa kuonekana tena wakizungumzia jambo hilo hadi janga jingine litokee.

Hivi majuzi, tabia hii ilionekana wakati mkasa wa moto ulipokumba wakazi wa mtaa wa Kijiji katika Kaunti ya Nairobi.

 

Mikakati

Viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Rais William Ruto, walifika katika eneo la mkasa na kueleza jinsi mikakati ilivyowekwa kuzuia hasara kubwa endapo mikasa kama hiyo itatokea katika siku za usoni.

Miongoni mwao ilikuwa ni ujenzi wa makao bora badala ya nyumba za mabanda zilizokuwepo, ujenzi kwa njia ambayo itatoa nafasi kwa barabara ili uokoaji urahisishwe kama kuna moto na pia usambazaji wa maji katika mitaa aina hiyo ili wakazi wenyewe wajisaidie kama kuna moto kabla maafisa wa idara ya zimamoto wawasili.

Mambo haya yote si mageni. Tumewahi kuyasikia kwa miaka na mikaka kwani mikasa ya moto katika mitaa ya mabanda hutokea mara kwa mara, si Nairobi pekee bali pia katika miji mingine nchini.

Ahadi na mikakati inayotolewa wakati wa mikasa aina hii haziwezi kusaidia kwa njia yoyote bila utekelezaji.

 

Mipango ya karatasi

Karibu kila kaunti huwa na mipango maalumu ya kuimarisha miji mikuu ingawa mipango hiyo husalia tu kwenye karatasi na vitabu.

Inafaa ikumbukwe kwamba mipango hiyo hunakiliwa na makundi ya wataalamu na watafiti ambao huduma zao hulipiwa kwa pesa za mlipa ushuru.

Tungekuwa na viongozi wanaojali maslahi ya wananchi, hivi sasa mitaa ya mabanda ambayo ndiyo wakati mwingi hukumbwa na mikasa mikubwa ya moto, ingekuwa imepungua pakubwa na badala yake kungekuwepo nyumba nadhifu kwa wananchi wenye mapato ya chini.

Kile kinachoturudisha nyuma ni siasa za ubinafsi ambapo wanasiasa hujali tu maslahi yao na yale ya wandani wao pekee huku wananchi wa kawaida wakisahaulika hadi mwaka wa uchaguzi ufike.

 

Ubinafsi

Wasomi wa masuala ya kisiasa wanaelewa fika jinsi wanasiasa hasa barani Afrika hupenda wananchi wawe maskini ndipo wafanikiwe kuwatumia jinsi watakavyo kufanikisha maazimio yao ya kibinafsi.

Ni kutokana na umaskini huu huu ambapo wanasiasa hupata njia rahisi ya kugawanya wananchi kwa misingi ya kikabila na vyama, mbinu ambayo imejikita mizizi humu nchini na inayotuletea madhara chungu nzima kila kukicha.

Kwa sasa serikali ya Jubilee imeweka wazi mipango yake ya kupambana na umaskini ikiwemo kwa kuwezesha wananchi kumiliki nyumba za kinadhifu.

Mpango huu ni mzuri ingawa mafanikio yake yatategemea zaidi uaminifu wa viongozi serikalini kuufanikisha.

You can share this post!

Mama akiona kuokota nywele katika kinyozi

TAHARIRI: Usiri wa wananchi wafaa kuheshimiwa

adminleo