• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Uhaba mkubwa wa damu wakumba Kenya

Uhaba mkubwa wa damu wakumba Kenya

Mkenya akitoa damu katika Hospitali Kuu ya Kenyatta katika Siku ya Kutoa Damu Duniani. Picha/ Evans Habil

Na BENSON MATHEKA na WANDERI KAMAU

Kwa Muhtasari:

  • Hakuna wakati Kenya imewahi kuwa na hifadhi ya kutosha ya damu. Kwa wakati huu kuna upungufu wa damu wa paini 251,000
  • Wakenya wengi wangali wanashikilia kwamba wanaweza kuambukizwa magonjwa, ikiwa watapokea ama kutoa damu. Wengine wanaongozwa na itikadi kali za kidini za kitamaduni
  • KNBTS inawataka Wakenya kuepuka tamaduni za jadi zinazowazuia kutoa damu
  • Kaunti zilizoathirika zaidi na uhaba wa damu ni Nairobi, Embu, Nakuru, Kisumu, Mombasa, Machakos, Kisii, Meru, Kericho, Nyeri, Garissa, Bungoma, Migori, Busia na Narok.

KENYA inakumbwa na uhaba mkubwa wa damu huku idadi ya watu wanaohitaji msaada wa damu kuokoa maisha yao ikiongezeka.

Maafisa wa kituo cha taifa cha kuhifadhi damu (KNBTS), wanasema idadi ya wanaojitokeza kutoa damu ni ndogo mno, huku mahitaji ya damu nchini yakizidi kuongezeka kutokana na idadi kubwa ya majeruhi wa ajali za barabarani, mashambulizi ya kigaidi na kuongezeka kwa wagonjwa wa saratani katika miaka ya hivi majuzi.

Katika kukabiliana na upungufu huo, KNBTS inawataka Wakenya kutumia siku ya Valentino mnamo Jumatano kutoa damu kwenye kampeni ya siku moja itakayoandaliwa katika kaunti mbalimbali.

 

Paini 251,000

Kulingana na mkurugenzi wa KNBTS, Dkt Josephine Githaiga, hakuna wakati Kenya imewahi kuwa na hifadhi ya kutosha ya damu. “Kwa wakati huu kuna upungufu wa damu wa paini 251,000,” asema Bi Githaiga.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), nchi inapaswa kuwa na paini 400,000 za damu kila wakati. Kiwango hiki kinaweza kufikiwa iwapo asilimia moja ya watu wangetoa damu mara moja kwa mwaka.

Dkt Githaiga anasema watu wazima nchini Kenya wanaogopa kutoa damu licha ya kuwa ndio wanaofaidika kwa wingi na damu hiyo.
“Hatujafikia viwango vya WHO kwa kuwa na paini 400,000 katika hifadhi yetu. Inasikitisha watu wazima hawatoi damu japo ni wao wanaofaidika kwa wingi na damu inayotolewa,” aeleza Dkt Githaiga.

Daktari huyo amekuwa akiongoza maafisa wa shirika hilo na washikadau kwenye kampeni ambayo KNBTS inalenga kukusanya paini 10,000 za damu siku ya wapendanao.

 

Sababu kuu

“Utoaji wa damu Kenya uko chini sana. Hii ni kwa sababu ya watu wazima kutopenda kutoa damu na pia watu kukosa kuelewa umuhimu wa kutoa damu,” alisema.

Mwaka huu, KNBTS imeamua kuhamasisha Wakenya kujitokeza kutoa damu kupitia mitandao ya kijamii vyombo vya habari na mabango.

“Lengo letu ni kuwaelimisha Wakenya kutoa damu kwa hiari mara kwa mara,” KNBTS ilisema kwenye taarifa.
Kulingana na shirika hilo, paini mbili kati ya kila paini tatu za damu huwekwa akina mama na watoto kuokoa maisha yao.

Ili kuwa na hifadhi ya damu ya kutosha, KNBTS inawataka Wakenya kuepuka tamaduni za jadi zinazowazuia kutoa damu.

KNBTS inashirikiana na mashirika ya BloodlLink Foundation, Shirika la Msalaba Mwekundu, Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Chama cha Madaktari na Wataalamu wa Meno (KMPDU), NHIF na AMREF miongoni mwa mengine katika juhudi za kuimarisha utoaji wa damu nchini.

 

Vikwazo vikuu

Kulingana na wataalamu, hofu ya kuambukizwa magonjwa, imani za kidini na misukumo ya kitamaduni ndivyo vikwazo vikuu vya uhaba wa damu nchini.

Kulingana na Bi Rachael Githiomi, ambaye ndiye Mkuu wa Shughuli za Ukusanyaji Damu katika Huduma ya Kitaifa ya Ukusanyaji Damu nchini (KNBTS) changamoto hizo ndizo wamekuwa wakikabiliana nazo katika juhudi za kuwahamasisha Wakenya kujitokeza kutoa damu.

“Wakenya wengi wangali wanashikilia kwamba wanaweza kuambukizwa magonjwa, ikiwa watapokea ama kutoa damu. Wengine wanaongozwa na itikadi kali za kidini za kitamaduni, zinazowaonya kuhusu ‘athari mbaya’ ikiwa watachanga damu yao kwa matumizi ya binadamu mwenzao,” asema Bi Githiomi.

Kaunti ambazo zinakumbwa na uhaba mkubwa ni Nairobi, Embu, Nakuru, Kisumu, Mombasa, Machakos na Kisii. Nyingine ni Meru, Kericho, Nyeri, Garissa, Bungoma, Migori, Busia na Narok.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Miguna aapa kurudi Kenya kwa lazima

Viongozi wa Kiambu wataka Ngilu akamatwe

adminleo