• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Nimewasamehe wote waliotaka nitemwe serikalini – Mwangi Kiunjuri

Nimewasamehe wote waliotaka nitemwe serikalini – Mwangi Kiunjuri

Waziri mpya wa Kilimo Bw Mwangi Kiunjuri akihutubu. Picha/ Maktaba

Na STEVE NJUGUNA

WAZIRI wa Kilimo Bw Mwangi Kiunjuri amesema hana chuki dhidi ya kiongozi yeyote katika kaunti ya Laikipia ama eneo la Mlima Kenya waliotaka atemwe serikalini. 

Bw Kiunjuri aliyekuwa akizungumza kwenye hafla ya mazishi ya Bw David Wokabi Muriithi, ambaye ni nduguye Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi, alisema amewasamehe waliomtakia mabaya.

Kwenye ujumbe ulioonekana kumlenga mbuge mwakilishi wa wanawake kaunti ya Laikipia, Bi Catherine Waruguru na viongozi wengine wa Mlima Kenya waliokuwa wamemhimiza Rais Uhuru Kenyatta asimjumuishe katika baraza lake la mawaziri, Bw Kiunjuri alisema madai ya kuwepo kwa chuki kati yake na viongozi hao ni dhana tu.

“Sijawahi kuchukia mtu yeyote. Ninataka kusema wazi hapa kwamba sina chuki dhidi ya mtu yeyote, na hasira inayosemekana ninayo kwa yeyote ni dhana tu,” akasema.

Awali kulikuwa na kampeni katika eneo la Mlima Kenya, huku sehemu ya viongozi wakiomba Rais Kenyatta kuzingatia kuacha Bw Kiunjuri nje ya baraza lake la mawaziri.

Viongozi walionyesha upinzani dhidi ya waziri huyo wakisema kuwa walikuwa wamepoteza imani kwake.

Hata hivyo Rais Kenyatta hivi majuzi alimteua Bw Kiunjuri ambaye alikuwa amehudumu  katika baraza la mawaziri katika kipindi cha kwanza kwa miaka mitatu na kumteua tena kwenye wizara ya Kilimo.

 

 

 

 

 

You can share this post!

China yaipa Kenya msaada wa mchele magunia 90,000

Wataalamu wa ICC kukutana Nairobi kuhusu utafutaji haki

adminleo